Tuesday, June 21

STEFANO: ABADILISHA ITIFAKI YA YESU MBINGUNI

Neno la Mungu linatuambia kwenye Wakolosai kwamba Yesu ameketi mkono wa kuume wa Mungu na kwenye Waebrania ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.

Wakolosai 3:1 Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.

Waebrania 12:2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.

Lakini nataka tujifunze kitu kuhusu Stefano mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu.

Matendo ya Mitume 6:5 Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;

Stefano alikuwa mtu aliyejaa:

i. Imani

ii. Roho Mtakatifu

iii. Neema

iv. Uwezo

Pia alikuwa na:

i. Hekima

ii. Ishara kubwa

iii. Maajabu makubwa

Hayo ni mambo ambayo Stefano alitambulika nayo. Ninachotaka ujifunze hapa sio hayo bali nataka uone unapomtendea Yesu kazi njema nini huwa kinatokea mbinguni.

Ukisoma kitabu cha Matendo ya Mitume utaona watumishi wa kwanza wakiitwa watu walioupindua ulimwengu.

Matendo ya Mitume 17:6 na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako,

Lakini Stefano hakuishia kuupindua ulimwengu tu, alifanya zaidi ya kuupindua ulimwengu.

Stefano alisababisha Yesu ambaye tunajua huwa ameketi mkono wa kuume wa Mungu, aache kuketi na kusimama.

Matendo ya Mitume 7:55 Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu.

Matendo ya Mitume 7:56 Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.

Yaani sijui kama unanielewa huyu jamaa amesababisha Yesu kwenda kinyume na itifaki, kuna viwango tukivifikia Yesu atatumia kufanya mambo makuu.

Upo tayari kutumikia? Jifunze kwa Stefano.

Ukijitazama umeshafikia kiwango hata cha kupindua hata familia yako tu?

🤐 Jisemee mwenyewe. Kama bado Lini utafika kiwango cha Stefano? Maana neno linatuambia tunatoka utukufu hata utukufu, tuna pokea neema juu ya neema.

2 Wakorintho 3:18 Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.

Yohana 1:16 Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.

Petro anakazia kwa kutuambia tukue katika neema lakini mara ngapi tumeng'ang'ania kukua katika sherida? Sisemi kwamba uachane na sheria hapana bali jivike upendo maana ndiyo kifungo cha ukamilifu.

2 Petro 3:18 Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele.

Wakolosai 3:14 Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.

Siri ya Stefano ilikuwa kwenye mambo manne imani, Roho Mtakatifu, uwezo na neema, alihakikisha anajawa na hivyo vitu vyote. Ngoja tuangazie mistari inayotuwezesha kupata hayo mambo manne.

IMANI:

Waebrania 12:2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.

Yesu ndiye mwenye kuanzisha na kutimiza imani yetu. Hakikisha imani yako inaazishwa na kutimiza na Yesu ili uweze kufika viwango ambayo Yesu anataka ufike.

Hii imani Yesu anaianzishaje na kuitimza? Ni kwa njia ya kusikia ambalo kuna kuja kwa kusikia neno lake.

Warumi 10:17 Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.

Kwa hiyo Stefano alikuwa mtu wa kulisikia neno la Kristo.

ROHO MTAKATIFU

Matendo ya Mitume 1:8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.

Waefeso 5:18 Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;

Stefano alihakikisha amepokea Roho Mtakatifu na amejazwa naye. Mstari hapo juu inatuonyesha umuhimu wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yetu ya kila siku.

Umempokea Roho Mtakatifu? Umejazwa na Roho Mtakatifu? Kama bado hakikisha unampokea na kujazwa naye. Kitendo cha kujazwa Roho Mtakatifu sio cha mara moja ni kitu endelevu, endelea kusoma Waefeso 5:19-21 utaona ni jinsi gani unaweza kujazwa Roho.

NEEMA

Luka 2:40 Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

Yohana 1:16 Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.

Yohana 1:17 Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.

Neno la Mungu linasema kwenye 1Petro 2:21 Yesu alituachia kielelezo tufuate nyayo zake, unaona hapa Stefano alinifunza maisha ya Yesu kwenye Luka 2:40 kwamba neema ya Mungu ilikuwa juu ya Yesu kwa hiyo alihakikisha na yeye ameipata hii neema.

Katika utimilifu wake tuna pokea neema juu ya neema na kujua kwamba neema ilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.

UWEZO

Luka 9:1 Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi.

Luka 24:49 Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.

Stefano alijua siri ya kupewa uwezo juu ya pepo wote na kuponya maradhi. Pia alikuwa amevikwa uwezo utokao juu. Unajua uwezo uliopewa na Yesu? Umejazwa na huu uwezo? Chukua hatua ndugu.

Tambua kwamba ukiweza kuyapata hayo mambo mannne kuwa na uhakika kwamba hekima utakavyokuwa nayo hamna anayeweza kushindana nayo, ishara na maajabu makubwa yataambatana na wewe.

Siri kuu ipo kwenye kusoma, kujifunza, kutafakari na kulishirikisha neno la Mungu. Maana ndipo utakapojua jinsi bora ya kuomba, kufunga, kukesha, utaua, kuridhika na mengine mengi.

Yesu anasema pasipo yeye sisi hatuwezi kufanya neno lo lote hakikisha unakaa ndani ya  mzabibu kama tawi.

Wewe sio wa kawaida Stefano alisababisha Yesu asimame toka kitini, Joshua alisimamisha jua, Ezekieli alifufua mifupa mikavu sana, mifupa ya Elisha ilifufua mtu, Eliya alizuia mvua isinyeshe kwa muda w miaka mitatu na miezi sita na hawa wote neno linatuambia walikuwa kama sisi.

Yakobo 5:17 Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.

Yakobo 5:18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.

Unasubiri nini?

Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia. Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako.

Nasema tena wewe sio wa kawaida.

Haleluya utukufu kwa Bwana Yesu.

Frank Riessen

0754809462


 

Thursday, March 3

NIANZIE WAPI?

 


Je hujui mahali pa kuanzia ili jambo unalolipanga lilete mafanikio kwako?

Inaweza kuwa hujui uanzie wapi kuhusu huduma, ndoa, biashara, kilimo, ufugaji, elimu, kutatua changamoto Fulani ya kimaisha na kadhalika, orodha inaweza kuwa ndefu sana. 

Kama hujui basi usiogope tulia suluhisho lipo hapa, kuna mambo manne muhimu ya kufanya ili mambo yaende vizuri.

 

1.    Maombi 


Wafilipi 4:6 Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.

 

Hatua ya kwanza kabisa ni kumjulisha Mungu hiyo haja yako kwa njia ya

Maombi. Acha kujisumbua kwa mawazo mengi yasiyokuwa na majibu, maana ukijisumbua neno la Mungu linasema kwenye Matayo “Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja?”. Rafiki tulia kwanza mwendee Baba yako wa mbinguni kwenye chumba chako cha siri, neno lake linasema ukiwa hapa sirini yeye anakuona na atakujazi (Matayo 6:6)

 

Bwana Yesu anatuhakikishia amani, ghafla ukiwa chumba cha siri unaona unapata amani ya ajabu, kufadhaika na hofu ulizokuwa nazo kuhusu hilo jambo lako vinatoweka ghafla kwa sabubu (Yohana 14:27). Sasa unapokuwa na amani ya Kristo utaona unaweza kufanya maamuzi sahihi kwa sababu amani ya Kristo moyoni mwako ndiyo inaaza kukuwezesha kuamua, utanza kupata mwelekeo wa kile unachotaka kufanya.

 

Ukiwa chumba cha sirini utaaza kuona ukaribu wa Mungu na kuu wake maana umemwita na umemfanya wa kwanza kwenye mipango yako kwani neno lake linasema kwenye Zaburi ukimwita anakuwa karibu na wewe.

 

Zaburi 145: BWANA yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu.


 

2.      Tafuta ushauri

 

Mithali 15:22 Pasipo mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika.

 

Msatri wetu hapu juu unatusisitiza umuhimu wa kupata ushauri kwa sababu pasipo ushauri wa kutosha makusudi ya mipango yetu ni vigumu kufanikiwa, lakini tukipata ushauri wa kutosha na sahihi makusudi ya mipango yetu yatafanikiwa.

 

Jitahidi kutafuta ushauri toka kwa watu waaminifu ambao hawatateka nyara wazo lako.Unaweza omba ushauri toka kwa viongozi wako wa kiroho, washauri wa bobezi wa hilo jambo lako, watu waliokutangulia kufanya unachotaka kufanya, makampuni ya ushauri waliosajiliwa na mamlaka za nchi.

 

Ukishapata ushauri wa kutosha anza kuchambua ushauri ulio bora ili uweze kuufanyia kazi, muda mwingine unaweza kuta kuna vipengele mbalimbali tofauti toka kwa washauri mbalimbali ambavyo inakubidi kuviunganisha ili kupata kitu kilicho bora, kwa hiyo sio vibaya kuchanganya ushauri A na B kupata kitu kilicho bora.

 

 

3.      Utafiti

Mithali 19:2 Tena si vizuri nafsi ya mtu ikose maarifa; Naye afanyaye haraka kwa miguu hutenda dhambi.

Hatua inayofuata ni kutoka sasa ndani na kwenda kufanya utafiti wa kile unataka kufanya, mstari wetu hapo unazungumzia maarifa. Unapfanya utafiti wa kitu unaazna kupata maarifa ya kile unaenda kufanya, kwenye utafiti utapata taarifa mbalimbali zinazoweza kukupa maarifa. 

Mfano unataka kuingia kwenye kilimo ni lazima ufanye utafiti wa maeneo bora kwa kilimo kwa kujua hali ya hewa, aina ya udongo, mazao yanayostawi hilo eneo, usafiri wa uhakika, aina za mbolea, muda wa kupanda, kupalilia, kuvuna, masoko ya kuuza mazao yako, bei za sokoni zipoje.

Je unataka kulima mazao ya aina gani ya muda mrefu au mfupi, mazao ya biashara au chakula, mazao yako ni ya kuuza ndani au nje ya nchi. Kwa hiyo taarifa zote za utafiti huu zitakusaidia kupata maarifa sahihi ya kuanza kufanya kilimo.

Neno la Mungu linasema kwenye kitabu cha Hosea 4:6 kwamba ‘watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa”. Na ili kupata maarifa lazima kufanya utafiti kwa kusoma vitabu, kujifunza kwa waliokutanglia tena wale waliofanikiwa, kwenda eneo la tukio na kujifunza mazingira yake.

 

4.      Tengeneza mpango wa biashara (Business plan)

 

Mithali 24:27 Tengeneza kazi yako huko nje, Jifanyizie kazi yako tayari shambani, Ukiisha, jenga nyumba yako.


Proverbs 24:27 (NLT) "Do your planning and prepare your fields before building your house.” 

Nimeweka huo mstari kwa lugha ya kingereza ili kurahisisha uelewa  maana kwenye Kiswahili pana ugumu kidogo wa kuelewa.

Mpango ni kitu muhimu sana kwenye maisha ya kila siku, sasa kuna hichi kitu kinaitwa mpango wa biashara huu mpango sio kwenye sekta ya biasha tu ndiyo unatakiwa uwepo, kimsingi kwenye kila eneo la maisha huu mpango unatakiwa uwepo au upo lakini unaweza kuwa na jina tofauti kidogo.

Kuna mahali Yesu anasema ukitaka kujenga mnara lazima ukae chini ufanye mahesubu kwanza kama unaweza kuumaliza au la.

Luka 14:28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? 29Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, 30wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza

Ni muhimu kuwa na mpango wa biashara ambao utakuwezesha kufanya jambo lako hatua kwa hatua mpaka utakapoona mafanikio. Kama hujui jinsi ya kuanda mpango wa biashara kuna watu au makampuni ambayo unaweza kwenda kwao na wakakupa hiyo huduma kwa gharama nafuu sana.

Naamini kwamba kwa sasa umepata mwanga wa mahali kwa kuanzia, maana ukimshirikisha Mungu ambaye ndiye chanzo hata la wazo la mpango wako, yeye huwa ana kawaida ya kutimiliza kile alichkiaanzisha moyoni mwako.

Wafilipi 1:6 Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;Mungu mwenyewe ndiye anayefanya kazi ndani yetu ili kutimiza kusudi lake jema.Wafilipi 2:13 Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.

 

 

 


Wednesday, September 22

SHALOM

Shalom mwana wa Mungu aliye hai.

Yohana 14:27 Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.
Neno Shalom (שלום) maana yake ni AMANI.
Shalom (AMANI) ni salamu ya jadi ya Kiebrania, lakini Shalom (AMANI) ya Yesu ni zawadi ya wokovu, ikimaanisha neema/fadhila za baraka za Kimasihi.
Shalom (AMANI) kama salamu ya jadi ya Kiebrania, Yesu katika mwili aliikuta na angeweza kabisa kutuachia hii Shalom ya Kiebrania kama salamu, lakini Yesu hakutuachia wala hakutupa Shalom (AMANI) ya salamu ya jadi ya Kiebrania bali alituachia na kutupa Shalom (AMANI) yake mwenyewe ambayo ni zawadi ya wokovu ikiwa na maana neema au fadhila za baraka za Kimasihi.
Yaani Yesu anatuambia hatoi AMANI kama ulimwengu utoavyo, najua ulishawahi kutana na watu wengi anasema ngoja niende ufukweni, mahali pa utulivu nisikilize na kimziki fulani kilaini hivi nirejeshe AMANI baada ya msongo wa wiki nzima kazini, kwenye biashara au kilimo, ndiyo wanakwenda na wanapata amani lakini baada ya muda akikumbana na changamoto za kimaisha ile AMANI inapotea, kwa hiyo inabidi atafute njia nyingine kuirejesha AMANI tena.
AMANI ya Yesu aliyotuachia na kutupa kamwe haipotei kwa sababu AMANI ya Yesu ni Yesu mwenyewe kwani neno la Mungu linatuambia Yesu ni Mfalme wa AMANI.
Isaya 9:6 Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.
Hii AMANI ya Yesu ipo ndani yako kwa sababu Yeye na Baba yake wanafanya makao ndani yako kwa sababu umempenda Yesu na kulishika neno lake.
Yohana 14:23 Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.
Kama hujampenda Yesu na kulishika neno lake nakushauri ufanye hivyo sasa, bofya kiungo hapo chini upate maelekezo ya kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako ili umpokee Roho Mtakatifu naye atakumiminia pendo la Mungu ndani yako ili uweze kumpenda Yesu. Kuna wengine inawezekana walikuwa wanasema tunampenda Yesu lakini ukweli ni kwamba huwezi mpenda Yesu pasipo kuwa na pendo la Mungu ndani yako ambalo linamiminwa na Roho Mtakatifu kwenye moyo wako.
Warumi 5:5 na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.
Huyu Shalom ndiye alikuwa na akina Shedraki, Meshaki na ABednego kwenye tundu la simba, anapokuwa ndani yako AMANI yako ni ya kudumu
Daniel 3:25 Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.
Nimekusalimu kwa salamu ya Kimasihi, na sio ile Shalom ya jadi ya Kiebrania.
Shalom, Shalom.



Sunday, May 2

NDIVYO MTU WA NDANI ANAVYOSIKIA NJAA AKIKOSA NENO.


Luka 2:36 – 37.

Niliwahi kufanya maombi ya kufunga siku fulani. Kadri ilivyokuwa inasogea jioni nilikuwa nasikia njaa sana ambapo kuna muda nilataka hata nifungulie kwa kula chochote, lakini ndani kabisa nilishuhudiwa kuendelea na kukamilisha. Nashukuru Mungu niliweza kumaliza ule mfungo vizuri, ila ukweli ni kwamba njaa niliyokuwa nayo haikuwa ya kawaida. Nimeshawahi funga mara nyingi kavu na siku nyingi kuliko hiyo siku lakini sikuwahi kuona njaa kama safari hii.

Jioni sasa ndiyo Roho Mtakatifu akanifundisha kwamba kwa jinsi huyu mtu wa nje alivyokuwa anasikia njaa ndivyo mtu wa ndani anavyosikia njaa ya NENO LA MUNGU asipolishwa. Taabu ile ile uliyopata kwa mtu wan je ya njaa ndivyo mtu wa ndani anavyosikia sema tu yeye ni mpole kwa hiyo hadai kwa nguvu kama huyu mtu wa nje anavyodai chakula na akilishwa anataka kupumzika. Mtu wa ndani akilishwa vizuri anapokea maagizo toka kwa Mungu na atafanya yale yanayompendeza Mungu.

Tazama jinsi mtu wa nje alivyowekewa ratiba ya lishe inayozingatiwa kwa umakini:

a.       Kifungua kinywa - Breakfast

b.       Chakula cha mchana - Lunch

c.       Chakula cha jioni - Supper

d.       Chakula cha usiku – Dinner

Tena saa nyingine anapangiwa maeneo maalumu ya kula nyumbani sebuleni, hotelini, mgahawani, beach n.k huku mkiongozana na wapendwa wenu. Mtu wa ndani hana ratiba ya kulishwa wala hana maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili yake, hana pia mtu wa kungozana naye kwenye kula chakula chake na wakati Roho Mtakatifu yupo.

Hivi Roho Mtakatifu ananiuliza ni wangapi wanaojenga nyumba zao wanakumbuka kujenga chumba maalumu cha kumlisha mtu wa ndani na maombi? Hapa wengi tutaangukia pua maana wengi wetu nyumba zetu zina vyumba maalumu kama vile study room, maktaba, sebule ya wageni maalumu, chumba cha mazoezi n.k lakini je kuna mwenye nyumba iliyojengwa au anayopanga kujenga ina eneo maalumu kwa ajili ya mtu wa ndani?

Kawaida ya wanadamu wengi tunampenda sana mtu wa nje kwani ana bajeti za kila namna za kumwezesha kuishi kwa raha, mifano japo michache:

a.       Chakula

b.       Vinywaji

c.       Burudani

d.       Likizo

e.       Sherehe

f.        Mavazi

g.       Malazi

h.       Elimu n.k.

Mtu wa ndani je naye hastahili kuwa na bajeti yake? Mifano michache tu:

a.       Biblia

b.       Ibada za Jumapili na nyinginezo katika wiki

c.       Vitabu vya watumishi waliopakwa mafuta na Bwana

d.       Semina

e.       Mikutano ya injili

f.        Warsha za injili

g.       Mikesha

h.       Elimu n.k

Tujiulize kati ya mtu wa ndani na wa nje ni yupi ambaye anapata mahitaji karibia yote japo nimetaja machache.

Wapendwa mtu wa ndani anaathirika sawa sawa na mtu wa nje anapokosa chakula. Kama mtu wa nje akikosa chakula anapata utapiamlo, magonjwa, udhaifu na mtu wa ndani pia anapata utapiamlo, magonjwa, udhaifu n.k.

Ni bora mtu wa ndani apate chakula chake kuliko wa nje maana sisi halisi ni mtu wa ndani wala sio wa nje. Mtu wa ndani akiwa vizuri wa nje naye lazima atakuwa vizuri.

Mungu akupe maarifa na ufunuo wa kumlisha na kumtunza mtu wa ndani katika jina la Yesu.

 

 

 

 


 

Saturday, May 23

NUHU AMEFUNGUA DIRISHA USIWE KAMA KUNGURU UTAPOTEA

Mwanzo 8:6

Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya;

Utangulizi:

Mstari wetu wa ufunguzi unaonyesha dirisha la safina likifunguliwa na Nuhu. Kama dirisha la safina linafunguliwa ina maana lilikuwa limefungwa kwa kusudi fulani na sasa lile kusudi limetimia.

Kusudi kubwa la dirisha la safina kufungwa ilikuwa ni kuwahifadhi hai Nuhu na jamaa yake yote na wanyama walio safi, na wanyama wasio safi, na ndege, navyo vyote vitambaavyo juu ya nchi kwa sababu ya maji ya gharika.

Kuna mambo kadhaa ninataka uyaelewe kuhusu huu mstari wa ufunguzi kwa mazingira yetu ya sasa. 

“Ikawa baada ya”inaonyesha muda fulani umepita kwenye tukio fulani.

“Siku arobaini”  kwa mazingira na muktadha wetu unasimamia kipindi fulani cha  muda tangu nchi iingie katika maombi ya siku tatu kumwomba Mungu atupiganie Watanzania dhidi ya gharika hii iliyoikumba dunia  mpaka siku tatu nyingine za kumshukuru Mungu kwa kutupigania.

“Nuhu” kwa mazingira yetu na muktadha wetu ni Rais wetu Dk John Magufuli. Pia litatumika kwa muktadha wa Nuhu halisi.

“Akalifungua dirisha” kwa mazingira yetu na muktadha wetu ni kufunguliwa kwa shughuli za kiuchumi na taasisi za elimu ziendelee tena upya.

“Safina” inawakilisha sehemu salama ambayo watu/viumbe vingine vinakaa kwa muda fulani kupisha maji ya gharika hapa tunaweza sema nyumbani au sehemu nyingine maalumu iliyoandaliwa kwa mausudi hayo.

“Alilolifanya” kwa mazingira yetu na muktadha wetu ni aina ya zuio lilokuwa limewekwa na mamlaka ya nchi kipindi gharika ilipoingia nchini mwetu.

1.      Dirisha limefunguliwa:

Kwa sasa tunaweza sema siku arobaini zimetimia na dirisha la safina yetu Watanzania limefunguliwa na Nuhu. 

Pamoja na Nuhu kufungua dirisha hakutoka nje moja kwa moja kuna tahadhari aliichukua ili kuhakikisha usalama wa familia yake, wanyama, ndege na vitambaavyo alivyokuwa nao. 

        i.        Tahadhari ya kwanza: 

Mwanzo 8:7

akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi.

Alimtoa kunguru kwenda kuangalia usalama huko nje, tunaona kunguru alikwenda huko na huko hata maji yakakauka juu ya nchi, hatuoni akirudi ndani ya Safina yamkini alipata matatizo na kupotea huko nje. 

Pamoja na kwamba dirisha limefunguliwa tahadhari bado ni muhimu kama mamlaka ile ile iliyofungua dirisha ambavyo inasisitiza. Bado tunasisitizwa kuchukua tahadhari bila kuacha kabisa.

Usipozingatia hutachelewa kupotea kama kunguru, ikawa hasara kwako, familia na taifa kwa ujumla. 

      ii.        Tahadhari ya pili:

Mwanzo 8:8

Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; 

Baada ya kunguru kupotea ilibidi Nuhu amtoe njiwa nje kuhakikisha usalama kama maji yamepungua usoni pa nchi. 

Bado ni muhimu kuchukua tahadhari tena na tena bila kuchoka, usifikiri Nuhu na familia yake hawakutaka kutoka nje, pamoja na mvua kuisha na dirisha kufunguliwa. 

Mtanzania endelea kutii maelekezo ya mamlaka iliyowekwa na Mungu, utaishi na usipoitii pamoja na maelekezo yake utapotea kama kunguru.

Kunguru alitakiwa kumtii Nuhu na kurejesha taarifa kwa Nuhu, lakini hakumtii Nuhu akapotelea alipopotelea.

Warumi 13:1

Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.

Sababu ya kutii mamlaka iliyo kuu ni kwamba hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu.  

Na ukimwasi mwenye mamlaka unakuwa umeshindana na Mungu na ukishindana na Mungu wajipatia hukumu. Haya sio maneno yangu ni maneno ya Mungu mwenyewe.  

Warumi 13:2

Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.

·      Utii wa njiwa

Mwanzo 8:9

bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani.

Tunaona njiwa anatii na kurejesha taarifa kwa Nuhu, na kuingizwa tena ndani. 

Mpendwa ukiona huwezi kufuata masharti ya kujikinga na gharika au huna sababu ya kutoka nje, endelea kukaa kwenye safina yako, haina haja ya kukimbilia kutoka dirishani kama kunguru na ukapotea. 

Rafiki nakusihi kama huwezi fuata tahadhari zilizowekwa na mamlaka zetu na huna kitu muhimu cha kukutoa ndani basi kaa tu humo kwenye safina, fuata njia ya njiwa ya kurudi kwenye safina usubiri tena siku kadhaa.

    iii.          Tahadhari ya tatu:

Mwanzo 8:10

Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili,

Hakuna ubaya binafsi ukangoja siku saba tena kabla ya kutoka nje ya safina yako, bado ndani ya safina kuna usalama tele.  

Kwani bado taarifa njema itakujia muda sio mrefu, saburi na uthabiti wa moyo ni muhimu katika mazingira kama haya ya majaribu, kwani tutapata tumaini. 

Yakobo 1:3

mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.

Warumi 5:4

na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; 

Haleluya naona saburi yako, naona uthabiti wa moyo wako na  naona tumaini ndani yako.   

Niliwahi kuandika “asubuhi yako lazima ije kwa uwezo wa Mungu”, nakuhakikishia kwamba hamna usiku usiokuwa na asubuhi, lazima kutapambazuka tu. Na tena usiku unapokuwa mzito ndiyo mapambazuko yako karibu sana. FURAHA ipo karibu sana, asubuhi yako inakuja.

Zaburi 30:5b

Huenda kilio huja kukaa usiku, Lakini asubuhi huwa furaha.

    iv.          Tahadhari ya nne: 

Mwanzo 8:10 - 11  

10 Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili,  11 njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi.

Njiwa anatumwa tena kuangalia usalama, safari hii njiwa analeta taarifa njema ambayo Nuhu angeweza kuitumia kutoka nje lakini bado aliendelea kukaa ndani ya safina. Kwenye hii vita taarifa njema zitakuja nyingi tu lakini bado ule wakati wa kujiachia mazima na bila tahadhari haujafika.

Pamoja na taarifa njema ambazo tutaendelea kuzipata kupitia mamlaka zetu bado tahadhari ni muhimu, tusiache kufuata miongozo ya kujikinga.

Njiwa alimletea Nuhu taarifa njema lakini Nuhu alisubiri ndani ya safina hakukurupuka kutoka na kujiachia kienyejienyeji.

Majani mabichi ya mzeituni tutayaona sana lakini bado nasisitiza tahadhari ni muhimu sana. Tutajua kwamba maji yamepunguka juu ya nchi lakini tahadhari ni muhimu.

      v.          Tahadhari ya tano:

 Mwanzo 8:12  

Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe.

Bado Nuhu alimtuma tena njiwa na njiwa hakumrudia tena kamwe, ni hakika njiwa hakupotea kama kunguru kwani tunaona alirudi na na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, kwenye Mwanzo 8:11 ina maana miti ilikuwa inaonekana kwa hiyo yamkini alipata makazi huko alikoenda. Lakini kumbuka Nuhu bado hakutoka nje, bado ni muhimu kutokutoka nje kama huna shughuli maalumu ya kufanya au huwezi kufuata masharti kwani nje maji ya gharika hayajakauka vizuri.

    vi.        Tahadhari ya sita:

 Mwanzo 8:13  

Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka.

Kwenye tahadhari hii Nuhu mwenyewe anashuhudia nje jinsi kulivyo kwa kufungua kifuniko cha safina. Nataka uone kuwa kuna tofauti kati ya dirisha la safina na kifuniko cha safina. Kupitia dirisha la safina Nuhu alikuwa haoni nje sawa sawa ndiyo maana aliwatoa kunguru na njiwa watoke wakaone, lakini kupitia kifuniko cha safina tuanaona Nuhu akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka. Hapa Nuhu angeweza kutoka maana nchi imekauka kuna mahali pa kukanyaga lakini bado hakutoka. Endelea kuchukua tahadhari bado kidogo kutakuwa na shwari kuu. Nuhu aliendelea tena kusubiri kwa mwezi mmoja na siku ishini na saba tena ili nchi iwe kavu kabisa na kupata uthibitisho na maelekezo rasmi ya kutoka nje toka kwa Mungu.

Mwanzo 8: 14  Na mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa kavu.


2.      Uthibitisho wa shwari kuu na maelekezo ya kutoka nje

 

Mwanzo 8:15-16

Mungu akamwambia Nuhu, akisema, Toka katika safina, wewe, na mkeo, na wanao, na wake za wanao pamoja nawe.

 

Mpendwa, Nuhu alichukua tahadhari sita kabla ya kuthibitishiwa na Mungu sasa hali ni shwari na wanaweza kutoka nje. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo Mungu kupitia amani ya mioyo yetu tunaweza kutoka nje bila tahadhari yoyote na kuishi kama zamani lakini pia inatubidi tuache kabisa yale yasiyomtukuza Mungu kuanzia ngazi zote yaani toka viongozi wote na wasio viongozi.

Kumbuka yale maombi ya siku tatu tulitubu kama Taifa na maana ya kutubu ni kugeuka kutoka katika njia mbaya na kufuata njia nzuri. Kumbuka tangazo la Rais liliambatana na andiko toka kwenye Neno la Mungu, mheshimiwa Rais hakukurupuka tu na maneno yake alipoagiza tutumie siku tatu za kumwomba Mungu wa rehema, alitumia hili neno.

2 Mambo ya Nyakati. 7:14

ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.


Watanzania tunatakiwa kuelewa Mheshimiwa Rais alitaka tuwe kama 2 Mambo ya Nyakati. 7:14 inavyosema kuhusu sisi na faida zake.


Kuhusu sisi Mungu anatutaka tujue:


·         Tumeitwa kwa jina la Mungu

·         Tuwe wanyenyekevu kwa Mungu

·         Tuwe waombaji

·         Tutafute uso wa Mungu

·         Tuziache njia zetu mbaya


Faida tunazopata toka kwa Mungu:


·         Mungu anatusikia toka mbinguni

·         Mungu anatusamehe dhambi zetu

·         Anaiponya nchi yetu


3.      Tukitoka tunatakiwa kufanya nini?


Mwanzo 8: 17  

Utoe pamoja nawe kila kilicho hai kilichomo pamoja nawe, chenye mwili, ndege, na mnyama, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi; wajae katika nchi, wawe na uzazi, wakaongezeke katika nchi.

 

Tunatakiwa tukamzalie Mungu matunda katika uzao wa wanadamu, uzalishaji wa mali za viwandani, kilimo, biashara, elimu yaani kwa kifupi tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuongezeka kwenye kila eneo la maisha yetu mpaka tuwe na ziada. Mungu anahitaji tuwe na maisha ya tija baada ya kutoka katika safina ndiyo maana anatuambia tuongezeke katika nchi, tafadhali ustafsiri tu ongezeko la kuzaana sisi wanadamu, ana maanisha ongezeko kwenye kila eneo halali la kila kitu halali vinavyomtukuza Mungu pekee.


4.      Shukurani zetu kwa Mungu


Mwanzo 8: 20  

Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.

 

Baada ya gharika Nuhu anatoa sadaka ya kumshukuru Mungu kwa NEEMA YA WOKOVU aliopewa na Mungu.


Mamlaka imetupa tena siku tatu za kumshukuru Mungu kwa ajili ya kutupigania na kutushindia dhidi ya gharika ya maji iliyotukumba.

Watanzania hatuna budi kumtolea Mungu wetu sadaka ya shukurani kwa Neema hii kuu ya wokovu dhidi ya gharika hii ya maji aliyotushindia.

Nuhu alikaa ndani ya safina kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa hiyo uzalishaji mali ulipungua sana, lakini hakuangalia upungufu aliokuwa nao bali alimwangalia Mungu na kumshukuru bila kujali upungufu uliotokea. Najua kwa muda huu tuliokuwa ndani ya safina kuna mapungufu tumeyapata lakini hii isituzuie kumshukuru Mungu kwa upungufu huo huo.


5.      Mungu anapokea sadaka zetu


Mwanzo 8: 21  

Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya.

 

6.      Ahadi ya Mungu kwetu

 

Mwanzo 8: 22  

Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.

 

Mungu anatuhaidi kwamba majira yote ya mwaka hayatokoma, iwe ni kwenye biashara, elimu, kilimo, kazi, sherehe na chochote kinachomtukuza yeye kilichokwama wakati wa gharika ya maji havitakoma.


7.      Hitimisho


Matayo. 10:16 b


basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.

 

Ni kweli Nuhu kafungua dirisha la safina lakini tahadhari bado ni muhimu kama mamlaka zinavyosisitiza. Unapoambiwa dirisha la safina limefunguliwa na tahadhari inasisitizwa pale pale jua mamlaka inajua dirisha sio sehemu rasmi ya kutoka nje. Kama itakulazimu kutoka kupitia dirishani kwa sababu maalumu basi usiache kuchukua tahadhari.


Amini kwamba saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo Mungu kupitia amani ya mioyo yetu tunaweza kutoka nje bila tahadhari yoyote kupitia mlangoni na hatutapotea kama kunguru. Kumbuka kwa sasa ni DIRISHA tu ndiyo limefunguliwa, MLANGO hauna muda mrefu Mungu atatupa RUHUSA RASMI ya kuufungua na kutoka nje, hii safari ni hatua.


Maisha ni lazima yaendelee, tukimtazama Yesu Kristo, usiyumbishwe ndugu songa mbele makelele ni mengi sana.


Wafilipi 3: 14  nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.


Frank Riessen,


0754809462