Tuesday, August 11

MAOMBI YA KUOMBA KWA KUTUMIA NENO LA MUNGU

Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

Waebrania 4:12. Neno la Mungu ni Mungu mwenyewe, Yeye ndiye msaada uliopo wakati wa taabu. Wakati tunapitia kwenye majaribu na mateso katika maisha yetu, omba NENO na maadui watakukimbia. Maadui wanamwogopa Mungu na neno lake, kwa sababu li hai, tena lina nguvu, na hata linadhuru na ni hatari. Hapa kuna baadhi ya maandiko ya maombi, ili kukusaidia maisha yako ya maombi, na kupata nguvu za kiroho katika kipindi cha udhaifu.

OMBA MAOMBI HAYA KILA SIKU ASUBUHI, MCHANA NA USIKU.

Baba umenipa funguo muhimu katika Mathayo 16:19 za kufunga na kufungua. Ninatumia funguo hizo kufunga na kufungua, kuvunja na kubamiza kila kitu ambacho kinazuia kutimizwa kwa mipango yako kamili katika maisha yangu. Ninaamuru na kutangaza kwamba kila mnyororo, kamba, gereza, pingu kwamba zimefunguliwa, zimekatwa, na kuondolewa kutoka kwenye maisha yangu katika jina la Yesu.

Baba, Bwana Nakushukuru, kwamba wewe pekee ndiye hakimu wa maisha yetu, kwa mujibu wa Yeremia 17:9-10 Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.

Baba naomba katika jina la Yesu, kwa mujibu wa Zaburi 22:19 Nawe, Bwana, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia. Baba naomba kwamba  utusaidie, na kutupa uvumilivu wa kusubiri  mapenzi yako kutimizwa.

 Baba katika jina la Yesu, neno lako liniasema katika Isa 41:10-12 usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako.

Baba, ninakubaliana na neno lako lenye nguvu, uweza, uhakika, na la kujiamini, kwamba utawalinda watu wako dhidi ya maadui. Umetuambia kwamba kisasi ni chako asema Bwana, na utawalipa waovu. Bwana Ninakushukuru, kwa ajili ya ulinzi wako, na neno lako la nguvu na la ukombozi. Katika jina la Yesu.

Baba tunakushukuru kwa neno lako linalosema katika Ayubu 5:12 Yeye huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao. Baba wa Mbinguni, ninachukua mamlaka ya neno lako kufunga, kufuta na kung’oa mipango yote miovu ya adui, nakuifanya kuwa utupu, batili, na kuifuta kwa jina la Yesu.

Baba katika jina la Yesu, umesema katika Zaburi 27:2 "Watenda mabaya waliponikaribia, wanile nyama yangu, watesi wangu na adui zangu, walijikwaa wakaanguka." Asante Bwana kwa ulinzi wako. Asante Bwana, kwasababu unatalnda.  Wakati maadui zetu wanakuja kula nyama yetu, tunakuwa dhaifu, tumelala kiroho, tumekata  tamaa, lakini uwezo wako katika damu umeruhusu maadui kuanguka ndani ya shimo la kuzimu. Asante Mungu wa huruma na neema, kwa upendo wako wa milele kwa watu wako.


Baba neno lako linasema nami katika Luka 10:19 kwamba “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.” Bwana natumia uwezo wako na mamlaka yako, ili kuvunja, kubamiza, kuponda, kung’oa, kutawanya vipande vipande, kila mipango ambayo shetani ameandaa dhidi ya maisha yangu, familia yangu, huduma yangu, nyumba yangu, uhusiano, fedha, na vitu vyote vilivyo vyangu. Nakushukuru Bwana, na ninadai ushindi kamili katika jina la Yesu.

Baba nasimama sawa sawa na neno lako katika Ayubu 6: 8 linalosema  “Laiti ningepewa haja yangu, Naye Mungu angenipa neno hilo ninalolitamani sana!” Bwana Naomba katika jina la Yesu kwamba ombi letu utalijibu kulingana na mapenzi yako na kwa wakati, na utatupa vitu vilivyomo katika mapenzi yako kwa ajili yetu.

Baba katika jina la Yesu kulingana na Wafilipi 4:6 unatuambia “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Bwana nakushukuru, kwamba tunaweza kuja kwako wakati wowote kwa maombi ili haja zetu zijulikane kwako.

Baba kama ulivyosema katika Zaburi 23:1 Wewe ni mchungaji wangu, sitapungukiwa au kukosa vitu vyovyote vizuri katika maisha yangu. Wewe ni Mungu ambaye unatupatia mahitaji yetu yote. Nakiri kama ulivyosema, kwamba huwezi kuzuia mambo yoyote mazuri kwa watoto wako. Baba nadai faida zako zote za kiroho, na za kimwili. Katika Jina la Yesu.

Baba umetuambia katika neno lako, katika Luka 17:6 kwamba “Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii.” Baba nachukua mamlaka ya neno lako leo, na kung’oa madeni yote ya kifedha, kila mapambano, kila misiba, kila ukosefu, uhitaji, na roho zote zinazoshambulia fedha zetu, afya, ndoa, nyumba, watoto, huduma, kazi zetu, na yote yaliyo yetu.  Nazifunga, nakuzing’oa  toka kwenye maisha yetu, na kuzitupa katika bahari. Katika jina la Yesu.

Baba umeniambia katika 2 Tim. 4:18 kwamba “Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina.” Baba nakushukuru kwa kuwa umeniokoa na kila matendo maovu ya adui, na kunihifadhi kwa ajili ya ufalme wako wa mbinguni. Baba ninasimama sawa sawa na neno lako na kuyafunga kila matendo maovu, yaliyofanywa maishani kwangu, watoto wangu, familia yangu, nyumbani kwangu, huduma yangu, afya yangu, fedha zangu, mustakabali wangu na vitu vyote tunavyomiliki. Ninayafunga toka mashariki, magharibi, kaskazini na kusini, mbingu ya pili, katika maji, kwenye moto, katika hewa, katika ardhi, katika maeneo, katika mazingira, na kila maeneo chini ya jua, mwezi, nyota, na sehemu nyingine zote za siri yanakojificha. Ninaachilia neno lako, damu ya Yesu, na jina lako dhidi yao, katika maeneo hayo yote, kwamba yatakuwa yamefungwa milele na milele amina.

Baba natumia funguo muhimu katika Mathayo 18:18 kwamba “na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.” Ninajifungua, pamoja na kila kitu changu, toka kila mnyororo, vifungo, pingu, na kamba katika jina la Yesu.

Baba kama ulivyosema katika kitabu cha Hesabu 11:1. Nasimama kwenye mamlaka ya neno lako, na amrisha moto ushuke kutoka mbinguni na kuharibu kila roho ya kurudi nyuma ambayo imewekwa na adui katika maisha yetu. Katika jina la Yesu.

Baba, Bwana nasimama sawasawa na neno lako katika Joshua 1:8. Naomba maneno yako yasindoke vinywani mwetu wala mioyoni mwetu, bali tuyatafakari mchana na usiku, ndipo tutakapoifanikisha njia yetu.

Bwana ninaomba mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, niyatafakari hayo sawasawa na neno lako, katika Wafilipi 4: 8.

Baba umeniambia katika 2 Timotheo 1:7 kwamba Mungu hakunipa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Baba napinga roho ya woga, nakataa kuwa na wasiwasi, au kukatishwa tamaa. Nautumia nguvu yako na mamlaka juu ya kila mipango na miradi ya adui. Nadai ushindi kamili juu ya nguvu zote za giza, katika jina la Yesu.

Baba neno lako linasema katika Yer 23:29 " Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande? Baba katika jina la Yesu, natumia moto wa Mungu kuteketeza kila uovu dhidi yangu, na wapendwa wangu, toka mashariki, magharibi, kaskazini na kusini. Natumia nyundo ya neno la Mungu kuvunja kila uovu wa vifungo vya nafsi, uhusiano wa damu, uchawi na laana zote mababu, uliopitia kwa uzao wetu. Najifunika, pamoja na kizazi cha pili, cha tatu na cha nne, kwa damu ya Yesu. Naachilia baraka za Bwana juu yetu, baraka za kizazi hadi kizazi, baraka za Ibrahimu, na baraka zote. Katika jina la Yesu.

Baba katika jina la Yesu. Navaa silaha zote za Mungu, napokea chapeo ya wokovu, navaa dirii ya haki kifuani, natwaa ngao ya imani, najifunga kweli kiunoni, nafungiwa miguu yangu utayari niupatao kwa injili ya amani na upanga wa roho ambao ni neno la Mungu kwa sala zote na maombi nikisali kila wakati katika Roho kwa mujibu wa Efeso 6: 10-18

Baba kwa mujibu wa neno lako katika Yer 30:17 Ulisema “Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema Bwana.” Nakushukuru kwa kutuponya machungu yetu, majeraha, makovu, na maumivu. Nakushukuru kwa ajili ya kuturejesha tena. Katika Jina la Yesu.

Baba katika Isa 53: 4-5, Ulisema “Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona." Bwana nakushukuru kwa neno lako, lina nguvu, linatupatia nguvu, ujasiri, ulinzi, na uponyaji katika jina la Yesu.

Baba nakushukuru, kama ulivyosema katika Zaburi 46:1 kwamba wewe ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Nakushukuru kwa kuwa tunaweza kukuita wakati wa shida.

Baba nasimama sawa sawa na neno lako katika Marko 3:27. Namfunga huyo mtu mwenye nguvu, nakuvunja kila vizuizi, kamba, vifungo, pingu, minyororo, minyororo ya utumwa, kutoka katika maisha yangu, wapendwa wangu, na yote yaliyo yangu. Ninaamrisha mali za mwenye nguvu kuharibiwa, sasa na hata milele. Katika jina la Yesu.

Baba nakushukuru kwa ulinzi wako, ulisema katika neno lako katika Kutoka 23:27 " Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao na kukimbia. Namshukuru wewe Bwana, kwa nguvu iliyopo katika neno lako ambayo husababisha maadui kuonyesha maungo yao na kukimbia. Katika jina la Yesu.
Baba katika jina la Yesu ninafungua machafuko na upofu wa mungu wa dunia hii, kutoka kwenye akili zetu, ambazo zinatuzuia kuona mwanga wa injili ya Kristo. Ninaita kila neno la Mungu linaloingia kwenye akili zetu, na moyo liinuke kwa nguvu ndani yetu.

Baba wa Mbinguni, asante ninakushukuru wewe, ninakutukuza wewe, ninakuabudu wewe, nakushukuru kwa neno lako katika Kumbukumbu 28:7 Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.  Asante kwa nguvu yako, ulinzi, na usalama ambao umetoa kwa watoto wako, tukitumia neno, maadui si tu watakimbia, bali watakimbia kwa njia saba kutoka kwetu, katika jina la Yesu.

Baba nakushukuru, kwa mikono yako imara, na mkono wako wa haki wa kulia. Umetuambia, katika 1 Petro 5: 7 Tumtwike yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu. Bwana nakushukuru kwa kujishughulisha na mambo yetu, nakushukuru kwa kuwa tayari  kwa ajili yetu wakati tunakuhitaji.

Baba katika jina la Yesu ninaliadhimisha jina lako; nakupa heshima na utukufu wote unaotoka kwenye jina lako takatifu. Neno lako linaniambia katika Joshua 1:5 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia kamwe wala sitakuacha.” Asante Bwana kwa ulinzi wako, na baraka.

Baba nakushukuru kwa neno lako katika 3 Yohana 1:2 linasema kwamba mipango yako kwa ajili yetu ni ya kutufanikisha, na kuwa na afya njema kama vile roho zetu zifanikiwavyo. Natumia mamlaka ya neno lako, na kudai ustawi, afya, furaha, mafanikio, amani ya akili, baraka, na kila mambo mema ambayo umepanga tupate, juu ya maisha yangu, wapendwa wangu, mali na vitu vyote nilivyonavyo, katika jina la Yesu.

Baba wa mbinguni neno lako katika Luke 8:11 linatuambia kwamba neno lako ni mbegu, na mioyo yetu ni ardhi. Bwana ninakuomba utayarishe mioyo yetu kupokea neno lako na kulificha katika mioyo yetu, tusitende dhambi dhidi yako, kwa jina la Yesu.

MAOMBI YA NENO YA UKOMBOZI TOKA KITABU CHA ZABURI

1.      Ee Mungu wangu, uniponye na adui zangu, Uniinue juu yao wanaoshindana nami. Zaburi 59:1

2.    Uwakomeshe kwa hasira, Uwakomeshe watoweke, Wajue ya kuwa Mungu atawala katika Yakobo, Na hata miisho ya dunia. Zaburi  59:13

3.      Ee Mungu, uniokoe, Maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu. Zaburi 69:1

4.   Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama. Na niponywe nao wanaonichukia, Na katika vilindi vya maji. Zaburi 69:14

5.      Amani na ikae ndani ya kuta zako, Na kufanikiwa ndani ya majumba yako. Zaburi 122:7

6.    Ubaya wao wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo na viuno Ndiye Mungu aliye mwenye haki. Zaburi 7:9

7.      Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. Zaburi 2:9

8.      Ee Mungu, usiwe mbali nami; Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia.  Zaburi 71:12

9.     Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe, Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye. Zaburi 7:1

1. Na jicho langu limewatazama walioniotea, Sikio langu limesikia habari za waovu walionishambulia. Zaburi 92:11

MAANDIKO YA MAOMBI YA UPONYAJI

1.      Zaburi 91:16 Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu.

2.      Zaburi  103:3 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.
Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote

3.      Yeremia 30:17 Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema Bwana, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye.

4.      Zaburi 118:17 Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya Bwana.
                                                     
5.    Yohana 10:10 Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.

6.      Zaburi 107:20 Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.

MAOMBI YA NENO YA MAJINA YA MUNGU

1.      Nalibariki jina lako Yehova -Yire — "Bwana atatupatia" (Mwanzo 22:13-14)

2.      Nalibariki jina lako Yehova -Rafa — "Bwana uniponyaye" (Kutoka 15:26)

3.      Nalibariki jina lako Yehova -Nisi— " Bwana ni bendera yetu" (Kutoka 17:8-15)

4.      Nalibariki jina lako Yehova -Shalom — "Bwana ni amani yetu" (Waamuzi 6:24)

5.      Nalibariki jina lako Yehova -Raah — "Bwana ni mchungaji wetu" (Zaburi 23:1)

6.      Nalibariki jina lako Yehova -Tsidkenu — "Bwana ni haki yetu" (Yeremia 23:6)

7.      Nalibariki jina lako Yehova -Shammah — " Bwana yupo hapa " (Ezekieli 48:35)
                                                                                                             
MAOMBI YA NENO YA KUAMRISHA VIUNGO VYA MWILI WANGU KUFANYA MAPENZI YA MUNGU

1.      Ee Bwana, naamuru mikono yangu kuinuliwa na kumtukuza Bwana kwa jina la Yesu

2.      Ee Bwana, naamuru mikono yangu kubarikiwa, kustawi, na kufanikiwa katika mambo yote yaliyoko katika mapenzi ya Mungu kwa ajili yangu katika maisha yangu. Katika jina la Yesu.

3.     Oh Bwana, naamuru macho yangu kukutazama wewe, ili kamwe nisipoteze lengo langu. Katika jina la Yesu.

4.      Ee Bwana, naamuru miguu yangu  kutembea katika njia ya haki, ambapo sitaogopa mabaya kwa jina la Yesu.

5.       Ee Bwana, naamuru masikio yangu kusikiliza mambo mazuri yenye ripoti nzuri.

6.     Ee Bwana, naamuru kinywa changu kuzungumza maagizo ya Mungu, neno la Baraka litoke kwenye kinywa changu.

7.       Ee Bwana naamuru mawazo yangu kuwafanywa upya kwa neno lako kila siku.

8.     Ee Bwana, naamuru mwili wangu mzima kutolewa kwako, kama dhabihu iliyo hai, takatifu, na wenye kukubaliwa kwenye huduma yako. Katika jina la Yesu.

MAOMBI KIMAANDIKO KWA BARAKA NA SHUKURANI

1.    Baba katika jina la Yesu nitashukuru kwa Bwana, kwa maana u mwema, upendo wako, na fadhili zako ni za milele

2.      Baba tunaomba utupe nguvu, na utubariki kwa amani katika jina la Yesu Zaburi 29:11

3.    Baba umetuambia kwamba utatuepusha na maovu yote na kuhifadhi maisha yetu. Bwana utaangalia kutoka kwetu, na kuingia kwetu, tangu sasa na hata milele

4.      Bwana nitakushukuru; Nitaliita jina lako, na kukufanya ujulikane kati ya mataifa kwa yale uliyofanya kwangu

5.      Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nasi sote. 2 Thes 3:18

MAOMBI YA VITA YA KUTUMIA ALAMA ZA MUNGU

Adui anakuja kuiba, kuua na kuharibu kila kitu chetu, ni lazima kuwa tayari kupambana na maadui, tujue silaha zetu, na kutumia neno la Mungu. Ni lazima kujifunza neno la Mungu na kulitumia katika maisha yetu ya kila siku.

Baba neno lako katika Yer 23:29 linasema “Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande? ”Nasimama sawa sawa na neno lako, na kuvunja vipande vipande kila mipango ya kishetani, miradi na kazi mbaya za adui, katika pepo nne za dunia, katika jina la Yesu.

Baba neno katika Waebrania 4:12 "linasema “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili. Nachukua mamlaka ya neno lako ambalo ni upanga na kugawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani ya kila nguvu za uchawi, kila enzi, falme, mamlaka, wakuu wa giza, mapepo wabaya katika ulimwengu wa roho, mishale ya moto ya adui, maadui wa siri, maadui wanaojulikana, mapepo ya utambuzi, maadui wa ndani, na mamlaka zingine zote za adui, kwa kuwafunga na kuwatupa katika shimo milele, katika jina la Yesu, Amina.

Baba neno lako katika Yer 23:29 linasema “Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande? ”. Natumia moto wa Mungu Mwenyezi, kuchoma kila kazi ya adui kama majivu. Chochote ambacho kilitumwa kwangu, kinachonifuata, kilichohamishiwa kwangu, au kwenye kitu chochote ambacho ni changu. Nazifunga, na kuzitupa katika lile ziwa la moto, sasa na hata milele, katika jina la Yesu.

Baba neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu Zaburi 119: 105. Nasimama sawa sawa na neno lako, na kutumia mwanga wako kuangaza kila mahali penye giza ambapo jua haliangazi. Naweka wazi kila matendo mabaya yanayotendeka kwenye maisha yangu, familia, watoto, fedha za nyumbani, kazi, huduma, ndoa, na yote ambayo ni yetu. Bwana nakushukuru kwa kufanya kazi za uovu wao kuwa dhaifu, zife, zifungwe na kufutwa, katika jina la Yesu.

Baba neno lako katika Yakobo 1:22-25 "linasema kwamba neno lako ni kama kioo" Natumia mamlaka ya neno lako, na kubamiza, kuangamiza vipande vipande vioo vyote vya mapepo, ambavyo adui hutumia kufuatilia maendeleo yetu, mafanikio, baraka, na yote yaliyo yetu. Naamrisha maadui, kuona shughuli zao mbaya, kushindwa, na anguko katika vioo  vyao vya kipepo, katika jina la Yesu.

Baba neno lako ni kama maji ambayo yatusafisha dhambi zote na uovu. Waefeso 5:26-27. Natumia maji ya Bwana Mungu mwenyezi kuwazamisha maadui, mafarao wote, mayezebeli, goliati na maadui wengine wote wa maendeleo yetu katika bahari Shamu, sawa sawa na Kutoka sura ya 15

Baba neno lako linaniambia katika Zaburi 107:20 "Kwamba neno ni kama dawa" Nasimama sawa sawa na neno lako ambalo ni kama dawa, na kuponya mioyo yetu na machungu yote, uponyaji wa kimwili, kiakili, kihisia, na kiroho. Naomba neno lako liturejeshee mara mia moja, kila kitu tulichopoteza, katika jina la Yesu

OMBA NENO ASUBUHI, MCHANA NA USIKU. OMBA NENO BILA KUKOMA. OMBA MPAKA UKOMBOZI UJE.







29 comments:

  1. MUNGU AKUBARIKI KWA MAFUNDISHO MAZURI

    ReplyDelete
    Replies
    1. Utukufu ni kwa NIKO AMBAYE NIKO

      Delete
    2. Mungu akubariki sana sana MTU wa Mungu. Hakika nimebariiwa sana. By Renatus 0752234601

      Delete
  2. Amen.barikiwa sana Mungu azidi kukuinua uendelee kugusa maisha ya wengine

    ReplyDelete
  3. Amen!ninazidi kubarikiwa na neno lako,Mungu akubariki muandaaji wa neno hili LA injili takatifu

    ReplyDelete
  4. Amen!ninazidi kubarikiwa na neno lako,Mungu akubariki muandaaji wa neno hili LA injili takatifu

    ReplyDelete
  5. Asante kwa mafundisho yenye kujengea Imani zetu na kutupa maongozo bora wa namna ya kuomba kwa kudai ahadi za Mungu kwetu. Tukiamini kuwa huwezi kutuahidi halafu asitupe, kumbe basi ni sisi wenyewe tunafanya maisha yetu kuwa magumu kwa kushindwa kuziishi ahadi za Mungu. Barikiwa sana mtumishi.

    ReplyDelete
  6. Bwana Mungu akuangazie nuru ya uso wake na kukuongeza siku zote za maisha yako. Ubarikiwe sana mtumishi kwa maombi haya uliyotuandalia.

    ReplyDelete

Barikiwa kwa ujumbe wako.