Sunday, May 2

NDIVYO MTU WA NDANI ANAVYOSIKIA NJAA AKIKOSA NENO.


Luka 2:36 – 37.

Niliwahi kufanya maombi ya kufunga siku fulani. Kadri ilivyokuwa inasogea jioni nilikuwa nasikia njaa sana ambapo kuna muda nilataka hata nifungulie kwa kula chochote, lakini ndani kabisa nilishuhudiwa kuendelea na kukamilisha. Nashukuru Mungu niliweza kumaliza ule mfungo vizuri, ila ukweli ni kwamba njaa niliyokuwa nayo haikuwa ya kawaida. Nimeshawahi funga mara nyingi kavu na siku nyingi kuliko hiyo siku lakini sikuwahi kuona njaa kama safari hii.

Jioni sasa ndiyo Roho Mtakatifu akanifundisha kwamba kwa jinsi huyu mtu wa nje alivyokuwa anasikia njaa ndivyo mtu wa ndani anavyosikia njaa ya NENO LA MUNGU asipolishwa. Taabu ile ile uliyopata kwa mtu wan je ya njaa ndivyo mtu wa ndani anavyosikia sema tu yeye ni mpole kwa hiyo hadai kwa nguvu kama huyu mtu wa nje anavyodai chakula na akilishwa anataka kupumzika. Mtu wa ndani akilishwa vizuri anapokea maagizo toka kwa Mungu na atafanya yale yanayompendeza Mungu.

Tazama jinsi mtu wa nje alivyowekewa ratiba ya lishe inayozingatiwa kwa umakini:

a.       Kifungua kinywa - Breakfast

b.       Chakula cha mchana - Lunch

c.       Chakula cha jioni - Supper

d.       Chakula cha usiku – Dinner

Tena saa nyingine anapangiwa maeneo maalumu ya kula nyumbani sebuleni, hotelini, mgahawani, beach n.k huku mkiongozana na wapendwa wenu. Mtu wa ndani hana ratiba ya kulishwa wala hana maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili yake, hana pia mtu wa kungozana naye kwenye kula chakula chake na wakati Roho Mtakatifu yupo.

Hivi Roho Mtakatifu ananiuliza ni wangapi wanaojenga nyumba zao wanakumbuka kujenga chumba maalumu cha kumlisha mtu wa ndani na maombi? Hapa wengi tutaangukia pua maana wengi wetu nyumba zetu zina vyumba maalumu kama vile study room, maktaba, sebule ya wageni maalumu, chumba cha mazoezi n.k lakini je kuna mwenye nyumba iliyojengwa au anayopanga kujenga ina eneo maalumu kwa ajili ya mtu wa ndani?

Kawaida ya wanadamu wengi tunampenda sana mtu wa nje kwani ana bajeti za kila namna za kumwezesha kuishi kwa raha, mifano japo michache:

a.       Chakula

b.       Vinywaji

c.       Burudani

d.       Likizo

e.       Sherehe

f.        Mavazi

g.       Malazi

h.       Elimu n.k.

Mtu wa ndani je naye hastahili kuwa na bajeti yake? Mifano michache tu:

a.       Biblia

b.       Ibada za Jumapili na nyinginezo katika wiki

c.       Vitabu vya watumishi waliopakwa mafuta na Bwana

d.       Semina

e.       Mikutano ya injili

f.        Warsha za injili

g.       Mikesha

h.       Elimu n.k

Tujiulize kati ya mtu wa ndani na wa nje ni yupi ambaye anapata mahitaji karibia yote japo nimetaja machache.

Wapendwa mtu wa ndani anaathirika sawa sawa na mtu wa nje anapokosa chakula. Kama mtu wa nje akikosa chakula anapata utapiamlo, magonjwa, udhaifu na mtu wa ndani pia anapata utapiamlo, magonjwa, udhaifu n.k.

Ni bora mtu wa ndani apate chakula chake kuliko wa nje maana sisi halisi ni mtu wa ndani wala sio wa nje. Mtu wa ndani akiwa vizuri wa nje naye lazima atakuwa vizuri.

Mungu akupe maarifa na ufunuo wa kumlisha na kumtunza mtu wa ndani katika jina la Yesu.

 

 

 

 


 

1 comment:

Barikiwa kwa ujumbe wako.