Tuesday, June 21

STEFANO: ABADILISHA ITIFAKI YA YESU MBINGUNI

Neno la Mungu linatuambia kwenye Wakolosai kwamba Yesu ameketi mkono wa kuume wa Mungu na kwenye Waebrania ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.

Wakolosai 3:1 Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.

Waebrania 12:2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.

Lakini nataka tujifunze kitu kuhusu Stefano mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu.

Matendo ya Mitume 6:5 Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;

Stefano alikuwa mtu aliyejaa:

i. Imani

ii. Roho Mtakatifu

iii. Neema

iv. Uwezo

Pia alikuwa na:

i. Hekima

ii. Ishara kubwa

iii. Maajabu makubwa

Hayo ni mambo ambayo Stefano alitambulika nayo. Ninachotaka ujifunze hapa sio hayo bali nataka uone unapomtendea Yesu kazi njema nini huwa kinatokea mbinguni.

Ukisoma kitabu cha Matendo ya Mitume utaona watumishi wa kwanza wakiitwa watu walioupindua ulimwengu.

Matendo ya Mitume 17:6 na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako,

Lakini Stefano hakuishia kuupindua ulimwengu tu, alifanya zaidi ya kuupindua ulimwengu.

Stefano alisababisha Yesu ambaye tunajua huwa ameketi mkono wa kuume wa Mungu, aache kuketi na kusimama.

Matendo ya Mitume 7:55 Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu.

Matendo ya Mitume 7:56 Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.

Yaani sijui kama unanielewa huyu jamaa amesababisha Yesu kwenda kinyume na itifaki, kuna viwango tukivifikia Yesu atatumia kufanya mambo makuu.

Upo tayari kutumikia? Jifunze kwa Stefano.

Ukijitazama umeshafikia kiwango hata cha kupindua hata familia yako tu?

🤐 Jisemee mwenyewe. Kama bado Lini utafika kiwango cha Stefano? Maana neno linatuambia tunatoka utukufu hata utukufu, tuna pokea neema juu ya neema.

2 Wakorintho 3:18 Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.

Yohana 1:16 Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.

Petro anakazia kwa kutuambia tukue katika neema lakini mara ngapi tumeng'ang'ania kukua katika sherida? Sisemi kwamba uachane na sheria hapana bali jivike upendo maana ndiyo kifungo cha ukamilifu.

2 Petro 3:18 Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele.

Wakolosai 3:14 Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.

Siri ya Stefano ilikuwa kwenye mambo manne imani, Roho Mtakatifu, uwezo na neema, alihakikisha anajawa na hivyo vitu vyote. Ngoja tuangazie mistari inayotuwezesha kupata hayo mambo manne.

IMANI:

Waebrania 12:2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.

Yesu ndiye mwenye kuanzisha na kutimiza imani yetu. Hakikisha imani yako inaazishwa na kutimiza na Yesu ili uweze kufika viwango ambayo Yesu anataka ufike.

Hii imani Yesu anaianzishaje na kuitimza? Ni kwa njia ya kusikia ambalo kuna kuja kwa kusikia neno lake.

Warumi 10:17 Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.

Kwa hiyo Stefano alikuwa mtu wa kulisikia neno la Kristo.

ROHO MTAKATIFU

Matendo ya Mitume 1:8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.

Waefeso 5:18 Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;

Stefano alihakikisha amepokea Roho Mtakatifu na amejazwa naye. Mstari hapo juu inatuonyesha umuhimu wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yetu ya kila siku.

Umempokea Roho Mtakatifu? Umejazwa na Roho Mtakatifu? Kama bado hakikisha unampokea na kujazwa naye. Kitendo cha kujazwa Roho Mtakatifu sio cha mara moja ni kitu endelevu, endelea kusoma Waefeso 5:19-21 utaona ni jinsi gani unaweza kujazwa Roho.

NEEMA

Luka 2:40 Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

Yohana 1:16 Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.

Yohana 1:17 Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.

Neno la Mungu linasema kwenye 1Petro 2:21 Yesu alituachia kielelezo tufuate nyayo zake, unaona hapa Stefano alinifunza maisha ya Yesu kwenye Luka 2:40 kwamba neema ya Mungu ilikuwa juu ya Yesu kwa hiyo alihakikisha na yeye ameipata hii neema.

Katika utimilifu wake tuna pokea neema juu ya neema na kujua kwamba neema ilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.

UWEZO

Luka 9:1 Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi.

Luka 24:49 Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.

Stefano alijua siri ya kupewa uwezo juu ya pepo wote na kuponya maradhi. Pia alikuwa amevikwa uwezo utokao juu. Unajua uwezo uliopewa na Yesu? Umejazwa na huu uwezo? Chukua hatua ndugu.

Tambua kwamba ukiweza kuyapata hayo mambo mannne kuwa na uhakika kwamba hekima utakavyokuwa nayo hamna anayeweza kushindana nayo, ishara na maajabu makubwa yataambatana na wewe.

Siri kuu ipo kwenye kusoma, kujifunza, kutafakari na kulishirikisha neno la Mungu. Maana ndipo utakapojua jinsi bora ya kuomba, kufunga, kukesha, utaua, kuridhika na mengine mengi.

Yesu anasema pasipo yeye sisi hatuwezi kufanya neno lo lote hakikisha unakaa ndani ya  mzabibu kama tawi.

Wewe sio wa kawaida Stefano alisababisha Yesu asimame toka kitini, Joshua alisimamisha jua, Ezekieli alifufua mifupa mikavu sana, mifupa ya Elisha ilifufua mtu, Eliya alizuia mvua isinyeshe kwa muda w miaka mitatu na miezi sita na hawa wote neno linatuambia walikuwa kama sisi.

Yakobo 5:17 Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.

Yakobo 5:18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.

Unasubiri nini?

Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia. Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako.

Nasema tena wewe sio wa kawaida.

Haleluya utukufu kwa Bwana Yesu.

Frank Riessen

0754809462


 

No comments:

Post a Comment

Barikiwa kwa ujumbe wako.