Saturday, May 23

NUHU AMEFUNGUA DIRISHA USIWE KAMA KUNGURU UTAPOTEA

Mwanzo 8:6

Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya;

Utangulizi:

Mstari wetu wa ufunguzi unaonyesha dirisha la safina likifunguliwa na Nuhu. Kama dirisha la safina linafunguliwa ina maana lilikuwa limefungwa kwa kusudi fulani na sasa lile kusudi limetimia.

Kusudi kubwa la dirisha la safina kufungwa ilikuwa ni kuwahifadhi hai Nuhu na jamaa yake yote na wanyama walio safi, na wanyama wasio safi, na ndege, navyo vyote vitambaavyo juu ya nchi kwa sababu ya maji ya gharika.

Kuna mambo kadhaa ninataka uyaelewe kuhusu huu mstari wa ufunguzi kwa mazingira yetu ya sasa. 

“Ikawa baada ya”inaonyesha muda fulani umepita kwenye tukio fulani.

“Siku arobaini”  kwa mazingira na muktadha wetu unasimamia kipindi fulani cha  muda tangu nchi iingie katika maombi ya siku tatu kumwomba Mungu atupiganie Watanzania dhidi ya gharika hii iliyoikumba dunia  mpaka siku tatu nyingine za kumshukuru Mungu kwa kutupigania.

“Nuhu” kwa mazingira yetu na muktadha wetu ni Rais wetu Dk John Magufuli. Pia litatumika kwa muktadha wa Nuhu halisi.

“Akalifungua dirisha” kwa mazingira yetu na muktadha wetu ni kufunguliwa kwa shughuli za kiuchumi na taasisi za elimu ziendelee tena upya.

“Safina” inawakilisha sehemu salama ambayo watu/viumbe vingine vinakaa kwa muda fulani kupisha maji ya gharika hapa tunaweza sema nyumbani au sehemu nyingine maalumu iliyoandaliwa kwa mausudi hayo.

“Alilolifanya” kwa mazingira yetu na muktadha wetu ni aina ya zuio lilokuwa limewekwa na mamlaka ya nchi kipindi gharika ilipoingia nchini mwetu.

1.      Dirisha limefunguliwa:

Kwa sasa tunaweza sema siku arobaini zimetimia na dirisha la safina yetu Watanzania limefunguliwa na Nuhu. 

Pamoja na Nuhu kufungua dirisha hakutoka nje moja kwa moja kuna tahadhari aliichukua ili kuhakikisha usalama wa familia yake, wanyama, ndege na vitambaavyo alivyokuwa nao. 

        i.        Tahadhari ya kwanza: 

Mwanzo 8:7

akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi.

Alimtoa kunguru kwenda kuangalia usalama huko nje, tunaona kunguru alikwenda huko na huko hata maji yakakauka juu ya nchi, hatuoni akirudi ndani ya Safina yamkini alipata matatizo na kupotea huko nje. 

Pamoja na kwamba dirisha limefunguliwa tahadhari bado ni muhimu kama mamlaka ile ile iliyofungua dirisha ambavyo inasisitiza. Bado tunasisitizwa kuchukua tahadhari bila kuacha kabisa.

Usipozingatia hutachelewa kupotea kama kunguru, ikawa hasara kwako, familia na taifa kwa ujumla. 

      ii.        Tahadhari ya pili:

Mwanzo 8:8

Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; 

Baada ya kunguru kupotea ilibidi Nuhu amtoe njiwa nje kuhakikisha usalama kama maji yamepungua usoni pa nchi. 

Bado ni muhimu kuchukua tahadhari tena na tena bila kuchoka, usifikiri Nuhu na familia yake hawakutaka kutoka nje, pamoja na mvua kuisha na dirisha kufunguliwa. 

Mtanzania endelea kutii maelekezo ya mamlaka iliyowekwa na Mungu, utaishi na usipoitii pamoja na maelekezo yake utapotea kama kunguru.

Kunguru alitakiwa kumtii Nuhu na kurejesha taarifa kwa Nuhu, lakini hakumtii Nuhu akapotelea alipopotelea.

Warumi 13:1

Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.

Sababu ya kutii mamlaka iliyo kuu ni kwamba hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu.  

Na ukimwasi mwenye mamlaka unakuwa umeshindana na Mungu na ukishindana na Mungu wajipatia hukumu. Haya sio maneno yangu ni maneno ya Mungu mwenyewe.  

Warumi 13:2

Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.

·      Utii wa njiwa

Mwanzo 8:9

bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani.

Tunaona njiwa anatii na kurejesha taarifa kwa Nuhu, na kuingizwa tena ndani. 

Mpendwa ukiona huwezi kufuata masharti ya kujikinga na gharika au huna sababu ya kutoka nje, endelea kukaa kwenye safina yako, haina haja ya kukimbilia kutoka dirishani kama kunguru na ukapotea. 

Rafiki nakusihi kama huwezi fuata tahadhari zilizowekwa na mamlaka zetu na huna kitu muhimu cha kukutoa ndani basi kaa tu humo kwenye safina, fuata njia ya njiwa ya kurudi kwenye safina usubiri tena siku kadhaa.

    iii.          Tahadhari ya tatu:

Mwanzo 8:10

Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili,

Hakuna ubaya binafsi ukangoja siku saba tena kabla ya kutoka nje ya safina yako, bado ndani ya safina kuna usalama tele.  

Kwani bado taarifa njema itakujia muda sio mrefu, saburi na uthabiti wa moyo ni muhimu katika mazingira kama haya ya majaribu, kwani tutapata tumaini. 

Yakobo 1:3

mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.

Warumi 5:4

na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; 

Haleluya naona saburi yako, naona uthabiti wa moyo wako na  naona tumaini ndani yako.   

Niliwahi kuandika “asubuhi yako lazima ije kwa uwezo wa Mungu”, nakuhakikishia kwamba hamna usiku usiokuwa na asubuhi, lazima kutapambazuka tu. Na tena usiku unapokuwa mzito ndiyo mapambazuko yako karibu sana. FURAHA ipo karibu sana, asubuhi yako inakuja.

Zaburi 30:5b

Huenda kilio huja kukaa usiku, Lakini asubuhi huwa furaha.

    iv.          Tahadhari ya nne: 

Mwanzo 8:10 - 11  

10 Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili,  11 njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi.

Njiwa anatumwa tena kuangalia usalama, safari hii njiwa analeta taarifa njema ambayo Nuhu angeweza kuitumia kutoka nje lakini bado aliendelea kukaa ndani ya safina. Kwenye hii vita taarifa njema zitakuja nyingi tu lakini bado ule wakati wa kujiachia mazima na bila tahadhari haujafika.

Pamoja na taarifa njema ambazo tutaendelea kuzipata kupitia mamlaka zetu bado tahadhari ni muhimu, tusiache kufuata miongozo ya kujikinga.

Njiwa alimletea Nuhu taarifa njema lakini Nuhu alisubiri ndani ya safina hakukurupuka kutoka na kujiachia kienyejienyeji.

Majani mabichi ya mzeituni tutayaona sana lakini bado nasisitiza tahadhari ni muhimu sana. Tutajua kwamba maji yamepunguka juu ya nchi lakini tahadhari ni muhimu.

      v.          Tahadhari ya tano:

 Mwanzo 8:12  

Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe.

Bado Nuhu alimtuma tena njiwa na njiwa hakumrudia tena kamwe, ni hakika njiwa hakupotea kama kunguru kwani tunaona alirudi na na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, kwenye Mwanzo 8:11 ina maana miti ilikuwa inaonekana kwa hiyo yamkini alipata makazi huko alikoenda. Lakini kumbuka Nuhu bado hakutoka nje, bado ni muhimu kutokutoka nje kama huna shughuli maalumu ya kufanya au huwezi kufuata masharti kwani nje maji ya gharika hayajakauka vizuri.

    vi.        Tahadhari ya sita:

 Mwanzo 8:13  

Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka.

Kwenye tahadhari hii Nuhu mwenyewe anashuhudia nje jinsi kulivyo kwa kufungua kifuniko cha safina. Nataka uone kuwa kuna tofauti kati ya dirisha la safina na kifuniko cha safina. Kupitia dirisha la safina Nuhu alikuwa haoni nje sawa sawa ndiyo maana aliwatoa kunguru na njiwa watoke wakaone, lakini kupitia kifuniko cha safina tuanaona Nuhu akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka. Hapa Nuhu angeweza kutoka maana nchi imekauka kuna mahali pa kukanyaga lakini bado hakutoka. Endelea kuchukua tahadhari bado kidogo kutakuwa na shwari kuu. Nuhu aliendelea tena kusubiri kwa mwezi mmoja na siku ishini na saba tena ili nchi iwe kavu kabisa na kupata uthibitisho na maelekezo rasmi ya kutoka nje toka kwa Mungu.

Mwanzo 8: 14  Na mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa kavu.


2.      Uthibitisho wa shwari kuu na maelekezo ya kutoka nje

 

Mwanzo 8:15-16

Mungu akamwambia Nuhu, akisema, Toka katika safina, wewe, na mkeo, na wanao, na wake za wanao pamoja nawe.

 

Mpendwa, Nuhu alichukua tahadhari sita kabla ya kuthibitishiwa na Mungu sasa hali ni shwari na wanaweza kutoka nje. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo Mungu kupitia amani ya mioyo yetu tunaweza kutoka nje bila tahadhari yoyote na kuishi kama zamani lakini pia inatubidi tuache kabisa yale yasiyomtukuza Mungu kuanzia ngazi zote yaani toka viongozi wote na wasio viongozi.

Kumbuka yale maombi ya siku tatu tulitubu kama Taifa na maana ya kutubu ni kugeuka kutoka katika njia mbaya na kufuata njia nzuri. Kumbuka tangazo la Rais liliambatana na andiko toka kwenye Neno la Mungu, mheshimiwa Rais hakukurupuka tu na maneno yake alipoagiza tutumie siku tatu za kumwomba Mungu wa rehema, alitumia hili neno.

2 Mambo ya Nyakati. 7:14

ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.


Watanzania tunatakiwa kuelewa Mheshimiwa Rais alitaka tuwe kama 2 Mambo ya Nyakati. 7:14 inavyosema kuhusu sisi na faida zake.


Kuhusu sisi Mungu anatutaka tujue:


·         Tumeitwa kwa jina la Mungu

·         Tuwe wanyenyekevu kwa Mungu

·         Tuwe waombaji

·         Tutafute uso wa Mungu

·         Tuziache njia zetu mbaya


Faida tunazopata toka kwa Mungu:


·         Mungu anatusikia toka mbinguni

·         Mungu anatusamehe dhambi zetu

·         Anaiponya nchi yetu


3.      Tukitoka tunatakiwa kufanya nini?


Mwanzo 8: 17  

Utoe pamoja nawe kila kilicho hai kilichomo pamoja nawe, chenye mwili, ndege, na mnyama, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi; wajae katika nchi, wawe na uzazi, wakaongezeke katika nchi.

 

Tunatakiwa tukamzalie Mungu matunda katika uzao wa wanadamu, uzalishaji wa mali za viwandani, kilimo, biashara, elimu yaani kwa kifupi tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuongezeka kwenye kila eneo la maisha yetu mpaka tuwe na ziada. Mungu anahitaji tuwe na maisha ya tija baada ya kutoka katika safina ndiyo maana anatuambia tuongezeke katika nchi, tafadhali ustafsiri tu ongezeko la kuzaana sisi wanadamu, ana maanisha ongezeko kwenye kila eneo halali la kila kitu halali vinavyomtukuza Mungu pekee.


4.      Shukurani zetu kwa Mungu


Mwanzo 8: 20  

Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.

 

Baada ya gharika Nuhu anatoa sadaka ya kumshukuru Mungu kwa NEEMA YA WOKOVU aliopewa na Mungu.


Mamlaka imetupa tena siku tatu za kumshukuru Mungu kwa ajili ya kutupigania na kutushindia dhidi ya gharika ya maji iliyotukumba.

Watanzania hatuna budi kumtolea Mungu wetu sadaka ya shukurani kwa Neema hii kuu ya wokovu dhidi ya gharika hii ya maji aliyotushindia.

Nuhu alikaa ndani ya safina kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa hiyo uzalishaji mali ulipungua sana, lakini hakuangalia upungufu aliokuwa nao bali alimwangalia Mungu na kumshukuru bila kujali upungufu uliotokea. Najua kwa muda huu tuliokuwa ndani ya safina kuna mapungufu tumeyapata lakini hii isituzuie kumshukuru Mungu kwa upungufu huo huo.


5.      Mungu anapokea sadaka zetu


Mwanzo 8: 21  

Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya.

 

6.      Ahadi ya Mungu kwetu

 

Mwanzo 8: 22  

Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.

 

Mungu anatuhaidi kwamba majira yote ya mwaka hayatokoma, iwe ni kwenye biashara, elimu, kilimo, kazi, sherehe na chochote kinachomtukuza yeye kilichokwama wakati wa gharika ya maji havitakoma.


7.      Hitimisho


Matayo. 10:16 b


basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.

 

Ni kweli Nuhu kafungua dirisha la safina lakini tahadhari bado ni muhimu kama mamlaka zinavyosisitiza. Unapoambiwa dirisha la safina limefunguliwa na tahadhari inasisitizwa pale pale jua mamlaka inajua dirisha sio sehemu rasmi ya kutoka nje. Kama itakulazimu kutoka kupitia dirishani kwa sababu maalumu basi usiache kuchukua tahadhari.


Amini kwamba saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo Mungu kupitia amani ya mioyo yetu tunaweza kutoka nje bila tahadhari yoyote kupitia mlangoni na hatutapotea kama kunguru. Kumbuka kwa sasa ni DIRISHA tu ndiyo limefunguliwa, MLANGO hauna muda mrefu Mungu atatupa RUHUSA RASMI ya kuufungua na kutoka nje, hii safari ni hatua.


Maisha ni lazima yaendelee, tukimtazama Yesu Kristo, usiyumbishwe ndugu songa mbele makelele ni mengi sana.


Wafilipi 3: 14  nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.


Frank Riessen,


0754809462


 

 

 

 

 

 


No comments:

Post a Comment

Barikiwa kwa ujumbe wako.