Thursday, December 5

UNIPE MLIMA HUU

Mwana wa Mungu ni wakati sasa wa kuchukuwa vilivyo vyako.

Leo tujifunze kwenye habari za Kalebu aliyesema kwa ujasiri UNIPE MLIMA HUU na akaudai kama urithi wake.

Kwenye somo hili utaelewa:

• Kwamba kama mtoto wa Mungu, Baba yako wa mbinguni amekuahidi urithi.
• Jinsi ya kuendelea kumiliki ahadi hizi za Mungu katika maisha yako.
• Jinsi ya kubaki kijana, mwenye nguvu, na uliyejaa imani katika safari yako hapa duniani.

Kama mwana wa Mungu unao urithi. Na kuujua urith wetu kama watoto wa Mungu ni muhimu sana.
Shetani hataki jujifunze kuhusu Neema na roho ya kufanyika wana kwa sababu itatusababisha tumiliki urithi wetu.

Wagalatia 4:1–7
1. Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote;
2. bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba.
3. Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia.
4. Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,
5. kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.
6. Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.
7. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.

Wagalatia 4 inazungumzia kuhusu urithi wetu na maana ya kuwa mwana na kumiliki urithi wetu.

Wagalatia 4:1-2 mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote;bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba.

Hapa neno mtoto linamaanisha ‘mchanga’ yaani kuna tofauti ya kuwa mtoto na mwana. Huwezi mpa mtoto gari lako aendeshe sio kwa sababu ana tabia zisizoridhisha ila ni kwa sababu ni mdogo (too young), lakini kuna umri unafika anakuwa mwana (amepevuka).

Nakumbuka wakati nilifika umri fulani Baba mdogo aliniita akaniambia sasa hivi Baba yako ni ndugu yako unaweza kuongea naye kama mtu mzima sio kama mtoto tena. 

Nilikuja gundua baadaye kwamba nipo kwenye daraja lingine la mahusiano na Baba yangu sio lile la kugombezwa kila saa au kuchapwa tena, bali tulikuwa tunakaa na kujadiliana mambo mbali mbali. Kumbe hapo sasa mimi nilikuwa ni mwana sio mtoto tena.

Wagalatia 4:3 Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia.

Kawaida za kwanza za dunia hapo anazungumzia sheria na kanuni ndiyo kusema amri 10.

Wagalatia 4: Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.

Pale tu tunapookolewa hatuwi tena chini ya SHERIA bali chini ya NEEMA ni wana sasa. Sio tena watoto.

Wagalatia 4 inazungumzia nafasi yetu kama wana mara tu tunapozaliwa mara ya pili.
Mara unapokuwa mwana unaweza kuchukua gari la Baba yako kwa sababu unao urithi unaoweza kuudai.

Kiasi gani cha urithi unachomiliki inategemea na kiwango gani unajua wewe ni mwana wa Mungu.
Wagalatia 4 inazungumzia nafasi yetu kama wana wa Mungu. Sio nafasi ambayo tunatakiwa kuitafuta bali ni nafasi amabayo tumepewa kwa sababu Yesu ametukomboa.

Yesu alikuja kumfunua Mungu kama "Baba."
Jina “Baba” ambalo Yesu alikuja kulifunua limebadilisha jinsi tunavyohusiana na Mungu.
Kabla Yesu hajaundea msalaba aliwatambulisha wanafunzi wake aina mpya ya maombi, kwenye Yohana 16.

Yohana 16:24 Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu (Jina la Yesu); ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.

Kabla ya hapa Yesu alikuwa amewafundisha wanafunzi wake jinsi ya kuomba sala ya Bwana (Baba Yetu uliye mbinguni), na wanafunzi walikuwa wameweza kuponya wagonjwa na kutoa mapepo n.k.

Kwa hiyo ni maombi gani haya mapya ambayo walikuwa hawajaomba hapo kabla? Haya ni maombi ambayo yamebeba Roho ya Mwana. Maombi "kwa jina la Yesu" ambayo humwona Mungu kama Baba.
Mungu anataka tumwone kama Baba, anataka tuwe na hisia za familia za upendo.

Hatuwezi kupata baraka za Agano Jipya na msimamo wa Agano la Kale na mawazo ya utumwa. Tunahitaji kujua kuwa sisi ni WANA, sio watumwa. Njia pekee tunayoweza kurithi ni kujua kuwa sisi ni wana.

Wagalatia 4 inahusu urithi: Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu kupitia Kristo.

Kuna urithi mwingi kwako wa kumiliki!

Mara nyingi katika Biblia, tunapewa aina mbili za watu ambao wanaonyesha tofauti kati ya maisha ya Mkristo aliyeshinda na maisha ya Mkristo aliyeshindwa. Na tunaweza kujifunza kutoka kwenye habari zao.

Mfano Abraham na Lutu; Abraham alikuwa mtu mwenye haki aliyeshinda na Lutu alikuwa mtu mwenye haki aliyeshindwa.

Lutu alikuwa mwadilifu lakini aligusa vitu vya ulimwengu ambavyo vilimwaathiri yeye na familia yake vibaya.

Kutokana na habari yake tunajifunza kwamba sio vyema kuleta vitu visivyofaa toka ulimwenguni na kuviingiza kwenye nyumba zetu, kwani vitaathiri familia zetu.
Mfano wa vitu hivyo ni magazeti ya udaku, kanda zisizo na maadili n.k.
Twende tu taratibu utanielewa tu muda sio mrefu.
Leo, tutaangalia wahusika wawili wa Bibilia ambao wanatuonyesha tofauti muhimu; nao ni Joshua na Kalebu.

Ilifika wakati Yoshua alikuwa Mzee na akaacha kumiliki urithi wake, wakati Kalebu hakuwahi kuwa Mzee na hakuacha kumiliki urithi wake.

— ‭‭Joshua‬ ‭11:23 Basi Yoshua akaitwaa hiyo nchi yote, sawasawa na hayo yote Bwana aliyokuwa amemwambia Musa; Yoshua naye akawapa Israeli kuwa ni urithi wao, sawasawa na walivyogawanyikana kwa kabila zao. Kisha nchi ikatulia isiwe na vita tena.

— ‭‭Joshua‬ ‭13:1 Basi Yoshua alipokuwa mzee, na kwendelea sana miaka yake, Bwana akamwambia, Wewe umekuwa mzee na kwendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa.

Je! Kuna kuna kutokupatana kati ya hiyo mistari miwili hapo juu? Hapana. Ni jambo moja kwenda vitani na kupigania ardhi. Na ni jambo lingine kupata kile ulipigania lakini usichukue umilki wake.

—Mithali 12:27a Mtu mvivu hapiki mawindo yake…

Kwa mfano, siku hizi, watu wana vitabu vingi vya Kikristo, mahubiri, DVD, CD, na maandiko (notes zile unazoandika kwenye kila semina na mikutano ya injili unayohudhuria) ya mahubiri. Lakini hawajilishi hizo rasilimali. Sio jambo la kutokuwa na muda wa kutosha. Ni suala la uvivu.

Panga wakati wa kusoma na kutumia vitabu vyote na rasilimali (materials) ambazo umenunua. Yatafakari, yatafune kipande kwa kipande.

Joshua aliteka ardhi yote ambayo Mungu alikuwa amewapa katika sura ya 11. Lakini katika sura ya 13, bado kulikuwa na ardhi zaidi ya kumiliki.

Wana wa Israeli hawakufurahia urithi ambao ulikuwa wao.

LEO MUNGU ANATUAMBIA KWAMBA KUNA URITHI MWINGI WA KUMILIKI

Usipomiliki ardhi ambayo ni yako, adui ataingia na kuimiliki. Hapa namaanisha ukishindwa kuchukua jukumu ambalo Mungu amekupa la kulea watoto wako na ukawaacha peke yao, adui ataingia na kuwafundisha, iwe ni kupitia ushawishi mbaya wa marafiki zao, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii n.k. Ongezea na mengine ambayo hujataka kumiliki.

- Yoshua 13: 6 na watu wote wenye kuikaa nchi ya vilima kutoka Lebanoni hata Misrefoth-maimu, maana, hao Wasidoni wote; hao wote nitawafukuza watoke mbele ya wana wa Israeli; lakini wewe uwape Israeli kuwa ni urithi wao, kama nilivyokuamuru.

Je bado kuna mashindano tunayopaswa kufanya hata baada ya ardhi kutekwa na tumepewa kama urithi? Ndio, lakini ni vita ya imani. Mashindano ya kumiliki kile ambacho ni chako tayari.
Mashindano yetu ni kumiliki kile ambacho tumepewa tayari na Mungu.

JINSI YA KUBAKI KIJANA, MWENYE NGUVU, NA ULIYEJAA IMANI ILI KUMILIKI URITHI WAKO.

Tukiwalinganisha Yoshua na Kalebu, tunapata siri ya kubaki kijana, kuwa na nguvu, na kuwa na imani na uwezo wa kumiliki urithi wetu.

Yoshua 13:1 Basi Yoshua alipokuwa mzee, na kwendelea sana miaka yake, Bwana akamwambia, Wewe umekuwa mzee na kwendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa.

Yoshua alizeeka. Lakini kulikuwa na mtu anakaribiana umri na Yoshua, kwa miaka 7 tu, ambaye hakuzeeka huyu si mwingine ni Kalebu.

Kuna cha kujifunza kutoka maisha ya Yoshua kwamba ikiwa utatumia maisha yako kupigana kila wakati, kila wakati ukisongwa (stress), utachoka na kuzeeka haraka sana.

Kalebu alibaki kijana. Kivipi?

Siri ya Kalebu ya kubaki kijana na kumiliki ardhi yake aliyohadiwa:

Yoshua 14:6 - 13
6 Wakati huo wana wa Yuda walimkaribia Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno Bwana alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea.
7 Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa Bwana aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu.
8 Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu, kwa utimilifu.
9 Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata Bwana, Mungu wako, kwa utimilifu.
10 Sasa basi, angalia, yeye Bwana ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu wakati huo Bwana alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano umri wangu.
11 Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani.
12 Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena.
13 Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake.

“Wewe wajua hilo neno Bwana alilomwambia (alilonena)” - Kalebu alilijua Neno la Mungu. Watoto wengi wa Mungu hawajui Neno la Mungu. Wanajua kile wahubiri wanasema. Lakini hawajui Mungu anasema nini. Jizoeze Neno la Mungu.

" katika habari zangu, na katika habari zako wewe " - Kalebu alijua kile Neno la Mungu lilisema juu yake. Leo hii tunasoma Bibilia kumwona Yesu, lakini pia kuona kile Mungu anasema maalumu kwa ajili yetu. Mungu anasema nini juu ya urithi wetu?

Urithi wetu katika Kristo:

Waefeso 1:3-14
3 Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;
4 kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.
5 Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.
6 Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.
7 Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.
8 Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi;
9 akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo.
10 Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo;
11 na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake.
12 Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu.
13 Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu.
14 Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.
“aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni” 

- Endelea kusoma hii mistari yote ili kuona baraka zote za kiroho ambazo Mungu ametupa.

" watu wasio na hatia mbele zake katika pendo." - Kwa sababu uko ndani ya Kristo, Mungu hukuona bila hatia. Sio tu kwamba anakuona bila hatia, lakini anakuona katika upendo. Mungu anakupenda.

" ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa " - Neno "ametuneemesha" ni neno linalomaanisha "neema kuu." Ni neno hilo hilo linamwelezea Mariamu ambaye Mungu alimchagua kuwa mama ya Yesu (Luka 1:28. ). Kiwango hicho hicho cha upendeleo ni chako. Na angalia huu mstari katika Waefeso 1: 6 hausemi "neema kuu katika KRISTO." Unasema "neema kuu kwa MPENDWA." Mungu anataka ujisikie unapendwa wakati unafikiria juu ya urithi wako, anataka ujisikie joto la upendo wake.

" Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi " - Neno "tunao", na lipo katika wakati uliopo. Inamaanisha kwamba tunatakiwa sasa (sio kesho) kushikilia kabisa huu ukweli kwamba tuna ukombozi kupitia damu yake na msamaha wa dhambi.

" sawasawa na wingi (utajiri) wa neema yake " - Umesamehewa sawasawa na utajiri wa neema ya Mungu- sio nje au mbali na utajiri wa neema yake. Hii inamaanisha kuwa kiwango kikubwa cha neema ya Mungu ni kiwango kikubwa cha jinsi ulivyosamehewa.

Soma kitabu cha Waefeso (haswa mlango wa 1) ili ujifunze juu ya urithi wako.

Turudi kwa Yoshua 14: 6–13: Siri ya Kalebu ya kubaki kijana na kumiliki ardhi yake ya ahadi.

" Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu " - Kalebu alikumbuka na kuutaja umri aliokuwa nao wakati aliacha kuzeeka. Hivi ulishawahi jiuliza ni lini uliacha kuzeeka? Kama hujaamua kuacha kuzeeka basi amua sasa wakati ndiyo huu. Tutaona huko mbele namaanisha nini ninaposema Kalebu aliacha kuzeeka, yamkini umeshajua kama umesoma Yoshua 14:6-13 kwa kutafakari.

"nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu" - Kalebu alikuwa na Neno la Mungu na ahadi moyoni mwake (Tafadhali soma Hesabu 14: 6-9). Aliyathamini maneno ya Bwana moyoni mwake. Urithi huo ulikuwa ndani ya Kalebu muda mrefu kabla ya Kalebu kuona huo urithi. Neno la Mungu lilikuwa moyoni mwake kabla mwili wake haujaona ahadi katika Neno la Mungu. Una habari gani ndani ya moyo wako kuhusiana na majitu unayokutana nayo kwenye maisha ya kila siku unapoiendea ahadi yako kuimiliki?

URITHI WAKO UNATAKIWA KUWA NDANI YAKO KABLA WEWE HAUJAWA NDANI YA URITHI.

" Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu, kwa utimilifu." - Kalebu alimfuata Bwana kwa utimilifu/ukamilifu wote.

" Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata Bwana, Mungu wako, kwa utimilifu." - Kalebu alijua kwamba hapiganii ardhi mpya; alikuwa anamiliki tu mali ambayo tayari ni ya kwake. Alielewa kuwa urithi aliohaidiwa tayari niwa kwake.

" Sasa basi, angalia, yeye Bwana ameniweka hai" - Kalebu alijua kuwa BWANA ndiye aliyemweka hai. Tunahitaji kujua kuwa ni Mungu ambaye anatuweka hai. Sio yale tunayofanya, sio mazoezi tunayofanya, sio madaktari tunaokwenda kutibiwa kwao, sio kufunga sana, sio sadaka tunazotoa bali ni Mungu mwenyewe anatuweka hai. Namwomba Mungu akuweke hai wewe unayesoma ujumbe huu ili uweze kurithi ahadi zako.

" tangu wakati huo Bwana alipomwambia Musa neno hilo " - Kalebu aliliamini kabisa neno la Mungu kupitia Musa kwamba watadai urithi wao. Wakati huo ndipo alipoacha kuzeeka. Aliamini hakika ahadi ya Mungu. Aliiweka moyoni mwake kabisa. Matokeo yake yalikuwa ni Mungu kumtunza Kalebu asizeeke na kumfanya hodari ili kumiliki urithi wake.

Hebu tuendelee tuone Kalebu anavyokiri ujana wake kwa kujiamini.

“Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani” - Kalebu alikuwa na nguvu za kivita, na nguvu za maisha ya kila siku. Hakuwa na nguvu za kiroho tu. Alikuwa na nguvu ya kimwili pia. 

Isaya 40:31 inasema, bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.

Hivi huwa unamngojea Bwana? Siku nyingine nita kuelekeza jinsi ya kumngojea Bwana ili upate nguvu mpya, upande juu kwa mbawa kama tai, upige mbio bila kuchoka na uende kwa miguu bila kuzimia.

Kalebu alikuwa anamiaka 85 wakati anamwambia Musa haya maneno “Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani” hicho ndiyo nasema kwamba Kalebu aliiacha kuzeeka siku akiwa na miaka 40 wakati Mungu anamuahidi urithi wake wa Hebron kupitia Musa.

Haijalishi umri kinachotakiwa ni kujua urithi wako, kukubali Mungu akutunze hai na kuufuatilia urithi wako.

" Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo " - Kalebu alikuwa na umri wa miaka 85 na bado alikuwa na nguvu, bado kijana. Mungu hakuwahi kumwambia Kalebu kwamba alikuwa mzee, lakini alimwambia Yoshua kuwa alikuwa mzee. Mungu alimfanya Kalebu kijana. Mungu aliliheshimu neno ambalo Kalebu alikuwa amelitunza moyoni mwake.

Je wewe ni kijana kwa muktadha huu? Kama ndiyo inuka udai mlima wako (Dai urithi wako).

" yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena." - Kalebu alijua kuwa Bwana alikuwa pamoja naye wakati wote.

Usiogope kwa jinsi Bwana alivyokuwa na Kalebu ndivyo alivyo pamoja na wewe sasa, kwani amesema:

Matayo 28:20b na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

Yohana 14:16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;

No comments:

Post a Comment

Barikiwa kwa ujumbe wako.