Thursday, November 28

UKWELI UNAOTAKASA

Yohana 17:17 Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.

Hamna aliyewahi kwenda kuoga bafuni, akaanza kuoga kwanza halafu ndiyo aingie bafuni kuoga. Tunaoga ndani ya bafu ili tutoke tukiwa wasafi.

Mwendee Yesu jinsi ulivyo yeye atakusafisha, hakuna anayeweza jisafisha ndiyo aende kwa Mungu akasafishwe, tunaenda wachafu kama tunavyoingia bafuni tukiwa wachafu na kutoka wasafi.

Kama bafu linaweza kusafisha miili yetu na ikawa safi basi si zaidi Yesu anaweza safisha roho zetu zikawa safi kuliko theluji.

Yesu ni zaidi ya bafu, kwa hiyo nenda kwake na uchafu wako atakusafisha na utakuwa msafi.

Hamna asiyemfahamu Mfalme Daudi na uchafu wake alioufanya lakini hakuwahi kujitakasa mwenywe bali alimkimbilia Mungu na kumwomba amsafishe naye atakuwa msafi kuliko theluji.

Zaburi 51:7 Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.

Kwa Yesu tunasafishwa na tunakuwa weupe kuliko theluji.

Sikia mtumishi wa Bwana ifuate injili inayotoka kwenye kiti cha Neema hiyo ndiyo inayokuhesabia haki tofauti na hapo haiwezekani ukahesabiwa haki.

2 Wakorintho 5:21 Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.

Waebrania 4:15 –16 Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.
16 Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

Ukijua kweli ya injili ya Neema utakuwa huru maana Neno la Mungu linasema mtaijua kweli nayo kweli itakuweka huru.

Yohana 8: 32 tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.

Mstari wetu wa ufunguzi unasema Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.

Tunatakaswa na Neno la Mungu ambalo ni Yesu Kristo mwenyewe, hakuna njia nyingine ya kutakaswa zaidi ya kazi iliyokamilika ya Yesu ya msalaba.

Epuka injili ya mlima Sinai kwani kamwe hutaweza kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria.

#Injili ya inayotoka kwenye kiti Neema inakuvuta kwa Yesu, bali injili inayotoka mlima Sinai inakuweka mbali na Yesu#

Soma Kutoka 19 - 20 uone Waisrael walivyoshindwa kuusogelea mlima wakati wanapewa sheria.

Hiyo siku haikuwa rahisi kwao.

Lakini sisi tunalo Agano Jipya la Yesu ambaye Mungu amemtoa kwa ajili yetu ili tusipotee bali tuwe na uzima wa milele.

Yohana 3:16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Mungu ametupenda tukiwa na dhambi kwa hiyo nenda kwake jinsi ulivyo usitafute kujitakasa wewe mwenyewe, wewe nenda tu atakutakasa mwenyewe.

1 Yohana 4:10 Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.

Kumbuka yeye ni mfinyanzi wewe ni udongo kwa hiyo anajua jinsi ya kukufinyanga zaidi ya unavyojuwa wewe.

Pia wewe ni kazi ya mikono yake, hakika hatakuacha lazima atakufinyanga mpaka uwe katika viwango vyake vya usafi.

Isaya 64:8 Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako.

Pokea kutakaswa kutoka kwa Yesu.

Frank Riessen

0754809462

No comments:

Post a Comment

Barikiwa kwa ujumbe wako.