Wednesday, December 11

MLANGO WA TUMAINI

Hosea 2:15 Nami nitampa mashamba yake ya mizabibu toka huko, na bonde la Akori kuwa mlango wa tumaini; naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri.
Mstari wetu wa ufunguzi unatuonyesha kuna kitu kinaitwa bonde la Akori, hii ni sehemu ambayo palitokea shida/mateso kwa familia ya Akani.
Akani pamoja na famila yake, mali na wanyama wake walipigwa kwa mawe na kutekeketezwa kwa moto, maana Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda, alitwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; hasira ya Bwana ikawaka juu ya wana wa Israeli (Yoshua 7:1).
Yoshua 7:24-26 Kisha Yoshua, na Israeli wote pamoja naye, wakamtwaa Akani, mwana wa Zera, na ile fedha, na Lile joho, na ile kabari ya dhahabu, na wanawe, na binti zake, na ng'ombe zake, na punda zake, na kondoo zake, na hema yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta juu hata bonde la Akori.
25 Yoshua akasema, Mbona umetufadhaisha hivi? Bwana atakufadhaisha wewe leo. Ndipo Israeli wote wakampiga kwa mawe, kisha wakawateketeza kwa moto, na kuwapiga kwa mawe.
26 Kisha wakakusanya juu yake chungu kubwa ya mawe hata leo; naye Bwana akauacha ukali wa hasira yake. Kwa sababu hiyo jina la mahali pale likaitwa, Bonde la Akori, hata hivi leo.
Pia mstari wetu wa ufunguzi unatuonyesha kuna kitu kinaitwa mlango wa tumaini.
Mungu anaweza kubadilisha mateso, shida, matatizo kuwa mlango wa tumaini na ukaishi maisha yenye mafanikio, furaha, shangwe na ustawi.
Mungu akufungulie milango ya matumaini kwenye huduma, ndoa, biashara, kazi, kilimo na watoto katika maisha yako.
Kuna watu wanafikiri wanapomkosea Mungu, Mungu anawavizia ili awaadhibu. Mungu ni wa rehema na neema unapomrudia anasema na yeye anakurudia, na haishii kukurudia tu bali anakufanya kuwa bora zaidi.
Mfano mzuri ni habari ya mwana mpotevu, alipozingatia moyoni mwake na kurudi kwa Baba yake tunaona jinsi alivyopokelewa, halikadhalika na sisi tunapozingatia mioyoni mwetu na kumrudia Mungu mbinguni inakuwa ni shangwe kuu.
Mungu anatambua udhaifu wetu ndiyo maana anasema wema wake unatuvuta ili tupate kutubu na anataka kila mmoja aifikie toba, hataki kumpoteza hata mmoja.
Ndiyo maana anageuza mabonde ya shida, matatizo kuwa milango ya matumaini.
Pamoja na kwamba bonde la Akori lilikuwa ni sehemu ya mateso lakini Mungu analigeuza sasa kuwa sehemu ya watu wa Mungu wanaomtafuta.
Isaya 65:10 Na Sharoni itakuwa zizi la makundi ya kondoo, na bonde la Akori mahali pa kulala makundi ya ng'ombe, kwa ajili ya watu wangu walionitafuta.
# Ni nyakati za kuburudishwa#

No comments:

Post a Comment

Barikiwa kwa ujumbe wako.