Wednesday, September 4

USIFE KABLA KIFO CHAKO


Shalom Kanisa.
Umekata tamaa? Huna tumaini? Hujui kesho itakuwaje? Umeletewa taarifa mbaya? Umetengwa? Unadharaulika?
Yamkini upo nje ya lango la mji kama wale wakoma wanne, mjini kuna njaa mbele kuna jeshi la Washami.
Umechanganyikiwa hujui uelekee wapi zaidi ya kuwaza kufa kama wale wakoma wanne.
Sikia huu ujumbe wa Bwana usife kabla ya kifo chako. Fanya maamuzi leo.
2 Wafalme 7:3-4
Basi walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe?
Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile. *Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami;* wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu.
Hawa wakoma wanne walifanya maamuzi ya kuliendea jeshi la Washami.
Siku zote palipo na ugumu (Washami) ndiyo penye fursa. Samaria kuna njaa ndugu wanakusubiri uliendee jeshi la Washami nao wafaidi.
Wakoma wanne walipata utajiri wa ghafla, waliweza kusababisha Waisrael wapate chakula na utajiri.
2 Wafalme 7:8
Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, *wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha;* wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha.
Mbona unasubiri hapo mlangoni hiyo biashara ife? Toka hapo mlangoni hiyo ndoa isife, huyo mtoto asife kwa madawa ya kulevya.
Songa mbele mawazo ya Mungu sio ya kwetu, hapo hapo unapoona unakaribia kufa, biashara/ndoa inakaribia kufa, Mungu anakuwazia mema.
Ona wakoma wanne walivyoamua kusonga mbele Mungu alikuwa ameshawaandalia mazingira ya kufanikiwa pamoja na ndugu zao waliowadharau.
Wanaokuzunguka wanakula mavi ya njiwa, wewe umeganda mlangoni.
Liendee jeshi la Washami mpendwa badilisha historia yako na ya wanaokuzunguka kama wakoma wanne.
Kamwe usikate tamaa mlango wa kutoka hapo ulipo upo. Neno linatuambia njia za kutoka mautini zina Yehova Bwana.
Zaburi 68:20
Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana.
Mkimbilie Mungu yeye ni msaada wetu ni msaada wakati wa mateso.
Zaburi 46:1
Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
Kumbe wakati wa mateso/changamoto/ magumu kuna msaasa unaoenekana tele wakati unapopita kwenye mikiki mikiki ya maisha.
Yesu anasema ulimwenguni tunayo dhiki lakini anasema ameushinda ulimwengu.
Yohana 16:33
Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.
Yesu anajua hapa ulimwenguni kuna dhiki lakini anasema tujipe moyo.
Jipe moyo ndugu yangu ushindi ni wa uhakika ndani ya Yesu.
Barikiwa na Bwana Yesu.
Frank Riessen.
0754809462

No comments:

Post a Comment

Barikiwa kwa ujumbe wako.