Bwana Yesu asifiwe
Kanisa.
Hesabu 25:1 – 5
Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja
na wanawake wa Moabu; 2kwa kuwa
waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu
wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao. 3Ikawa
Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za BWANA zikawaka juu ya
Israeli. 4Kisha BWANA akamwambia Musa, Watwae wakuu wote wa hao watu,
ukamtungikie BWANA watu hao mbele ya jua, ili kwamba hizo hasira kali za BWANA
ziwaondokee Israeli.
Mistari yetu ya ufunguzi inaonyesha mafanikio makubwa kwa Mfalme
wa Moabu dhidi ya Waisrael.
Maana alifanikiwa kuwachonganisha Waisrael na Mungu wao na WIVU
wa Mungu uliwaua Waisrael ishirini na nne elfu.
Unapozungumzia Israel ni taifa teule la Mungu lililotolewa Misri
kwa mkono wa Mungu ulio hodari na wenye nguvu.
Kumb
26:8
Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu;
Hawa ndugu walikwa wana ulinzi wa Mungu wa hali ya juu sana
wazungu wanasema (Top security and well protected) lakini walimkosea Mungu kwa
KUTOKUKATA TAMAA kwa Mfalme wa Moabu aliyeitwa Balaki.
Ipo mifano mingi sana kwenye Biblia ya watu wema waliofanikiwa
kwa kutokukata tamaa na kusukuma maombi yao mpaka wakapata matokeo. Kwenye somo
hili natumia mfano wa mtu mbaya kufundishia.
Ukianzia na sura ya 22 ya kitabu cha Hesabu utaona Mfalme Balaki
alivyowaogopa wana wa Israel nakutaka Baalamu awalaani ili awafukuze katika nchi
yake.
Hesabu 22: 1 – 6
1 wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi tambarare za
Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko.
2 Na Balaki mwana wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli
wamewatendea Waamori.
3 Moabu akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu
akafadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli.
4 Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu
litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya
mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile.
5 Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori,
ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema,
Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena
wanakaa kunikabili mimi.
6 Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana
nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke
katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye
umlaaniye hulaaniwa.
Kwa hiyo kutokea hapo Mfalme Balaki alimwajiri Balaamu ambaye
alikuwa ni mganga maana mstari wa 7 wa Hesabu tunaambiwa Wazee wa Moabu na
Midiani walichukua ujira wa uganga
mikononi mwao kwenda kwa Balaamu.
Balaki
alituma ujumbe kwa Balaamu mara mbili, yaani ujumbe wa kwanza uliposhindwa
kumleta Balaamu kwa Balaki, bado Balaki hakukata tamaa akatuma ujumbe wa pili
mkubwa, wenye cheo zaidi na ujira mkubwa zaidi.
Ujumbe wa
pili ulifanikiwa kumleta Balaamu kwa Balaki.
Hesabu
22: 7 -12 (Ujumbe wa kwanza)
7 Wazee
wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi
mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki.
8 Akawaambia,
Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana atakavyoniambia; wakuu
wa Moabu wakakaa na Balaamu.
9 Mungu
akamjia Balaamu, akasema, Ni watu gani hawa ulio nao pamoja nawe?
10 Balaamu
akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema,
11 Tazama,
kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu
hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza.
12 Mungu
akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana
wamebarikiwa.
Hesabu
22: 15 – 21(Ujumbe wa pili)
15 Basi
Balaki akatuma wakuu mara ya pili, wengi zaidi, wenye cheo wakubwa kuliko wale
wa kwanza.
16 Wakamfikilia
Balaamu, wakamwambia, Balaki mwana wa Sipori asema hivi, Nakusihi, neno lo lote
lisikuzuie usinijie;
17 maana
nitakufanyizia heshima nyingi sana, na neno lo lote utakaloniomba nitalitenda;
basi njoo, nakusihi, unilaanie watu hawa.
18 Balaamu
akajibu akawaambia watumishi wa Balaki, Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa
fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, Mungu wangu,
kulipunguza au kuliongeza.
19 Basi
sasa nawasihi, kaeni hapa tena usiku huu, nipate kujua Bwana atakaloniambia
zaidi.
20 Mungu
akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda
pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi.
21 Balaamu
akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.
Tunajifunza
hapo kutokukata tamaa na gharama kubwa aliyoiingia Balaki kumpata Balaamu.
Yamkini Balaki angekata tamaa kwenye jaribio lake la kwanza maana ni Mungu
ndiye aliyemzuia Balaamu asiende kwa Balaki, lakini bado Balaki alituma ujumbe
mwingine mkubwa zaidi na wenye cheo zaidi kuliko ule wa kwanza bila kujali kuwa
kikwazo alikuwa ni Mungu mwenyewe.
Mara
ngapi vikwazo vidogo vidogo tu vimekuzuia usifikie ndoto/hatma yako? Kwa
taarifa yako Balaki alizuiwa ndoto yake na Mungu mwenyewe lakini bado hakukata
tamaa aliendelea kusukuma maombi yake
Umewahi
kujiuuliza ni mara ngapi umekata tamaa baada ya jaribio la kwanza kushindwa
yaweza kuwa ni huduma, biashara, ndoa, malezi, kazi,elimu ulipofanya jambo
Fulani kwenye hayo maeneo ukashindwa na kuishia hapo hapo.
Na hayo
yote kuna gharama kubwa umetumia kuyafanya lakini haukufanikiwa, sikiliza mwana
wa Mungu aliye hai wewe ni bora kuliko Balaki, tuma tena maombi kwa ajili ya
hiyo kazi, anza tena hiyo huduma, anzisha biashara tena upya, usichoke kuiombea
hiyo ndoa yako, usimkatie tamaa huyo mtoto mtafutie shule nyingine, mpe mtaji
mwingine lakini kumbuka safari hii ongeza bidii kwenye maombi, kufunga,
kumtolea Mungu pasipo kuchoka hakikisha ujumbe wa sasa wa kupeleka maombi yako
kwa Mungu ni mkubwa kuliko ule wa kwanza.
Hebu
tuendelee kujifunza kwa Balaki ambavyo hakukata tamaa. Baada ya Balaamu kufika
kwa Balaki na kuelezwa haja ya Balaki, Balaamu alimpa Balaki masharti magumu na
ya kutumia gharama kubwa sana lakini Balaki hakuchoka aliyatekeleza yote.
Ikawa asubuhi Balaki akamchukua Balaamu, akampandisha hata
mahali pa juu pa Baali; na kutoka huko akawaona watu, hata pande zao za mwisho.
Huu
mstari wa 41 nataka ujifunze kitu Fulani hapa, najua mara nyingi huwa tunakuwa
tumeshayaona mafanikio ya kihuduma, biashara, kazi, ndoa, watoto n.k kama
Balaki alivyowaona wana Waisrael toka mahali pa juu.
Sisi
mahali petu pa juu ni kwenye maombi na huko huwa tunaona mafanikio yetu, shida
ni kwamba tunakata tamaa, tunachoka kusukuma maombi mpaka jambo lizaliwe kwenye
ulimwengu wa mwili, yamkini umeona ndoa, huduma, biashara, kazi, watoto na
mengine mengi ukiwa mahali pa juu (Maombi) lakini havijawa halisi kwenye
ulimwengu wa mwili.
Usichoke
kuyasukuma kwa maombi mpaka yatokee, jenga madhabahu hapo nyumbani, kazini,
kwenye biashara, kwenye huduma na toa sadaka utaona yale uliyoyaona ukiwa
mahali pa juu yakitokea kwenye maisha yako.
Balaki
alijenga madhabahu saba, na kutoa sadaka ya ngombe saba na kondoo saba mara
tatu. Kwa hiyo alijenga jumla ya madhabahu 21, alitoa ngómbe 21 na kondoo 21.
Hiyo ni
gharama kubwa sana Balaki aliingia na mara zote toka anatuma ujumbe Mungu ndiye
alikuwa anawatetea wana wa Israel kwa kumzuia Balaamu asiende na hata Balaki
alipotoa sadaka zote hizi bado ni Mungu alikuwa anamwambia Balaamu awabariki
Waisrael.
Gharama
ya ibada ya Balaki haikuwa ndogo, ilikuwa kubwa maana ilijumlisha kupanda
vilima na kujenga madhabahu na kutoa sadaka za wanyama, na bado atakuwa aalikuwa
akimlipa Baalaamu ujira wa uganga mkubwa tu.
Hesabu
23: 1 – 2 (Madhabahu na sadaka za kwanza)
1 Balaamu
akamwambia Balaki, Nijengee hapa madhabahu saba, ukaniandalie hapa ng'ombe
waume saba, na kondoo waume saba.
2 Balaki
akafanya kama Balaamu alivyonena. Balaki na Balaamu wakatoa sadaka, ng'ombe
mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.
Hesabu
23:15 – 16 (Madhabahu na sadaka za pili)
15
Akamwambia Balaki, Simama hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami
nitaonana na Bwana kule.
16 Bwana
akaonana na Balaamu akatia neno kinywani mwake, akasema, Umrudie Balaki,
ukaseme hivi.
Hesabu
23: 28 – 30 (Madhabahu na sadaka za tatu)
28 Basi Balaki akamchukua Balaamu akaenda naye
mpaka kilele cha mlima Peori, mahali paelekeapo upande wa nyika iliyo chini
yake.
29
Balaamu akamwambia Balaki, Haya, unijengee hapa madhabahu saba, kisha
uniandalie ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba.
30 Basi Balaki
akafanya kama Balaamu alivyosema, akasongeza sadaka ng'ombe mume na kondoo mume
juu ya kila madhabahu.
Balaki
alijua kabisa kwamba Mungu ndiye alikuwa anmzuia Balaamu asiwalaani Waisrael
lakini bado aliendelea kusukuma maombi kupitia ibada ya madhabahu na sadaka.
Hivi ulishawahi kujiuliza wewe ni mara ngapi umepeleka maombi yako kwa Mungu
tena kwa kuyasindikiza na sadaka kubwa na bado yakakwama lakini badala ya
kuendelea kungángánia umekata tamaa na kusimama njia panda na kuanza kulalamika
yaani kama ni sadaka huyo mtoto nimemtolea lakini Mungu hajajibu, yaani hii
ndoa nimeiombea we acha tu, mh hii biashara nimeshazunguka makanisani na kwa
watumishi kibao lakini wapi bado mambo hayaendi ni hasara tu.
Ndugu
yangu Balaki hakukata tamaa pamoja na Mungu kuwa mtetezi wa Israel bado jamaa
aliendelea kutoa sadaka na kujenga madhabahu. Wewe ni mwana wa Mungu na Mungu
anasema amekubariki kwa Baraka zote za rohoni ndani yake Yessu Kristo, Mungu
hana mpango wa kuzuia maombi yako kama alivyoyazuia ya Balaki.
Waefeso
1:3-4
3
Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote
za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;
4 kama
vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe
watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.
Umechaguliwa
ndani ya Kristo hii ni haki yako usikate tamaa, usichoke kusukuma maombi ili kuchukua hizo baraka ili mradi iwe ni
katika mapenzi ya Mungu.
Alichokuwa
akiomba Balaki hakikuwa katika mapenzi ya Mungu, mapenzi ya Mungu kwa Waisrael
ni kubarikiwa na sio vinginevyo.
Ukisoma
Hesabu sura ya 24, 23 na 24 mpango mzima wa Balaki ulishindwa lakini
tunapoingia sura ya 25 tunaona Balaki akifanikiwa kuwakosanisha wana wa Israel
na Mungu wao kwa chakula, zinaa na ibada ya sanamu.
Bwana
Yesu asifiwe kama huyu mwovu aliweza kuliangusha taifa teule kwa kutokukata
tamaa kwa nini wewe mwenye haki wa Mungu unashindwa ?
Balaki alibadilisha gia angani akatumia
wanawake wa Moabu kuwashinda adui zake
Hesabu
25:1-2
1 Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu
wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu;
2 kwa
kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao;
watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao.
Msatri wa
pili “kwa kuwa waliwaalika’’ hapa anazungumzia wanawake wa Moabu waliawaalika
Waisrael.
Tusome
andiko hili kwenye Biblia Habari Njema (BHN) utanielewa vizuri.
Hesabu
25:1-2
1Waisraeli
walipokuwa huko Shitimu, wanaume walianza kuzini na wanawake wa Moabu. 2Wanawake
hao waliwaalika Waisraeli washiriki matambiko waliyotambikia miungu yao, nao
Waisraeli wakala chakula na kuiabudu miungu yao.
Mpendwa wangu badilisha gia angani kama Balaki, anza kumtumia
Roho Mtakatifu katika maombi yako kwani yeye ni msaidizi wetu. Naona hunielewi,
neno linasema Mwanamke ni msaidizi wa mwanaume, maana yake sio kwamba msaidizi
hana nguvu/uwezo, la hasha ana nguvu na uwezo mkubwa tena kukushinda, bado
hujaelewa kasome habari za Samson utaelewa na pia hii habari ya wanawake wa
Moabu walivyoweza kuwaangusha Wana wa Israel.
Sisi tunaye Msaidizi ambaye ni bora kuliko wanawake wa Moabu.
Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui
kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza
kutamkwa.
Wao
wanataja wanawake wa Moabu, wao wanataja mtaji mkubwa wa biashara, wao wanataja
uzoefu mkubwa wa kazi lakini sisi tunalitaja jina la Bwana.
Ulishawahi
kutaka kuingia kwenye biashara fulani uakona utakavyoambiwa, wewe unakuja na
mtaji mdogo hivyo, mtu Fulani alishindwa, unaaza biashara ya genge kwa elimu
yako hiyo utaweza wewe kweli, utaweza kweli kulipa kodi za serikali vizuri
wewe, na kelele nyingi za aina hiyo.
Lakini nakwambia kamwulize Daudi uzoefu
wake ulikuwa kuchunga kondoo, kupigana na samba na dubu na mtaji wake ulikuwa
kombeo tu lakini alishimshinda Goliati wake.
Usiogope
Goliati wako kwa maana yupo ili uwe Mfalme, bila Goliati hakuna Ufalme. Sukuma
maombi yako, pambana kwenye maombi.
Zaburi
20: 7-8
7 Hawa
wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu.
8 Wao
wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama.
Mpendwa
Bwana Yesu asifiwe yamkini umekwama mahali hujui ufanye nini, hamna msaada
popote, ninachoweza kukwambia songa mbele kama wale wakoma waliodharaulika
walivyosonga mbele wakisema ikiwa ni kufa na tufe, ikiwa ni kuishi na tuishi,
na ghafla walipofika kwenye kambi ya Washami waliwakuta Washami wamekimbia
wameacha kambi yao na kila kitu.
Hawa
wakoma walitajirika ghafla na Waisrael wakapata chakula cha kutosha.
2 Wafalme
7: 3-5, 8
3 Basi
walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona
tunakaa hapa hata tufe?
4
Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa
hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami;
wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu.
5 Basi
wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na
walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu.
8 Basi
wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja,
wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda
wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua
vitu, wakaenda, wakavificha.
Hivi hawa
walikuwa wanhesabika kuwa ni najisi waliweza kusonga mbele, hawakukata tamaa
waliweza kutajirika na kuwezesha wana wa Israel kupata chakula badala ya mavi
ya njiwa kwanini wewe uliye ndani ya Kristo ushindwe?
Acha kula
mavi ya njiwa kwa gharama kubwa songa mbele ingia kambi ya Washami utajirike na
kupata chakula cha kutosha hatimaye wanaokuzunguka nao wafaidi.
Wewe ni
zaidi ya mshindi, unayaweza yote katika yeye akutiaye nguvu na aliyeko ndani
yako ni mkuu kuliko yeye aliye nje.
Balaki
kama nilivyosema hakukata tamaa mpaka mwisho, baada ya mbinu ya kwanza
kushindwa alibadili mbinu akatumia mbinu ya mafundisho na mwalimu wake hakuwa
mwingine zaidi ya Mganga Balaamu.
Neno
linasema watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. (Kwa faida tu soma mstari
wote wa 6 wa Hosea 4, usiishee njiani kama tulivyozoea malizia wote uone hasara
ya kukosa maarifa mahali inaishia) Ukijua kosa tunalolifanya kwa kukosa maarifa
unaweza kulia maana madhara yake ni mabaya sana.
Hosea 4:6
Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako
.
Hivi wewe huoni ajabu huyu jamaa aliamua kukaa
darasani na kusaka maarifa ya jinsi ya kuwaangamiza Waisrael? Kwa nini usikae
darasani kwa Roho Mtakatifu upate maarifa ya kutokuangamizwa?
Kwa nini unakaa
kwenye baraza ya wenye mizaha (Zaburi 1) na kuanza kuwasimulia watu magumu ya
noda yako, watoto wako, biashara yao, huduma yako, elimu yako n.k.
Balaki aliamua kukaa chini ya mafundisho ya Balaamu
Mganga na akafanikiwa, wewe mwana wa Mungu mwenye baraka zote za rohoni,
uliyechaguliwa kabla ya misingi ya dunia, Yesu akakufia, Yesu akakupa Roho
Mtakatifu, Yesu akakupa jina lake, damu yake na unazo silaha zote za Mungu pale
kwenye Waefeso 6 ni nini kinakushinda usikae chini ya Mwalimu Roho Mtakatifu
akakupa maarifa ya kufanikiwa pale unapokwama?
Ufunuo wa Yohana 2:14
14 Lakini ninayo
maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya
Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba
wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.
Hebu omba hii sala fupi Mungu akupe maarifa
(Hebu ifanye kuwa sehemu ya ombi lako kwa kila siku na kwa mtu mwingine ambaye
unataka apewe maarifa ya Mungu):
Waefeso 1:17-23
17 Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa
utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye;
18 macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue
tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake
katika watakatifu jinsi ulivyo;
19 na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu
tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake;
20
aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa
kuume katika ulimwengu wa roho;
21 juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na
nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali
katika ule ujao pia;
22 akavitia vitu vyote chini ya miguu yake,
akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo
23 ndilo mwili wake, ukamilifu wake
anayekamilika kwa vyote katika vyote.
Kuna Kiongozi fulani wa nchi fulani aliwahi
kusema hili neno mara tatu ELIMU ELIMU ELIMU alichokuwa anasisiza ni umhumu wa
ELIMU kwa wananchi wa taifa lake, nami leo nakwambia MAARIFA YA MUNGU, MAARIFA
YA MUNGU MAARIFA YA MUNGU.
HITIMISHO:
Mafanikio ya Balaki tunayaona kwenye Hesabu 25:1 – 5. Ila soma sura zote kuanzia Hesabu 22, 23,24 na 25 kwa
makini.
Kuanzia sura ya 22 mpaka 24 Balaki hakufanikiwa, tunakuja kuona
mafanikio yake kwenye sura ya 25.
Hesabu 25 inaanza kwa kuonyesa tu mafanikio ya kuwakosesha
Israel kwa Mungu na hatimaye kuangamizwa kwa watu 24,000 kwa wivu wa Mungu.
Na
siri ya mafanikio yake ni kutokukata tamaa, kusukuma maombi na kuwa mbunifu
baada ya mbinu ya kwanza kushindwa.
Yawezekana bado unatumia mbinu za kutegemea kuombewa na watu
wengine (Kuombewa sio kubaya ila unatakiwa ukuwe na wewe uombee wengine), au kuomba siku ya Jumapili tu ukienda kanisani na mbinu nyingine
ambazo hazijakusaidia ni wakati sasa wa kubadili mbinu.
Unabadili vipi mbinu? Nenda kwa Roho Mtakatifu atakufundisha mbinu
mpya.
Balaki alifanikiwa katika maaeneo yafuatayo kuwakosanisha
Waisrael na Mungu wao:
- Zinaa ya kimwili
- Sadaka walizowachinjia miungu yao
- Uzinzi wa kiroho (Kuabudu miungu mingine)
Hesabu
25: 1-2
1 Basi
Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu;
2 kwa
kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao;
watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao.
Na
mafanikio haya yanatokana na mafundisho ya Balaamu ya utoaji wa sadaka ulio
bora, zinaa na kuabudu sanamu.
Ndugu
yangu tujitahidi kupata mafundisho sahihi ya maarifa ya Mungu ili tuweze kupata
mafanikio katika mambo yote.
3 Yohana
1:2
Mpenzi naomba
ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako
ifanikiwavyo.
Frank Riessen
0754809462
No comments:
Post a Comment
Barikiwa kwa ujumbe wako.