Naona kuna vitu viwili
tunashindwa kutofautisha katika haya mambo tunayojadili/changia, vitu hivyo ni
1.
Dini iliyoasisiwa na mtu kumtafuta Mungu
2.
Ufalme wa Mungu/Mbinguni uliorejeshwa na
Yesu kumrejesha mtu kwa Mungu (Wokovu).
DINI ILIYOASISIWA NA
MTU KUMTAFUTA MUNGU
Dini
inamaanisha jumla ya imani ya binadamu kadhaa pamoja na mafundisho wanayotoa
kuhusu yale ambayo wanayazingatia ama kuyasadiki, yaani mambo ya roho, kama vile kuhusiana na Mungu, maisha na uumbaji.
Kwa misingi hiyo tunaona kwamba dini zote zinafanana katika
malengo yao ya kumtafuta Mungu. Kwa hiyo kwa ujumla Dini ni mpango wa mtu
kumtafuta Mungu. Sasa basi katika huu mpango wa mtu wa kumtafuta Mungu kunakuwa
na namna tofauti tofauti za kumfikia huyo Mungu na zote kwa mtazamo wa mtu ni
sahihi hazina shida.
Dini ni matokeo ya njaa ya roho ya mwanadamu ambayo mtu bado
hajaweza kuifafanua ila bado anatafuta ili ajiridhishe njaa yake ya rohoni
(satisfaction). Njaa hii isiyokuwa na ufafanuzi inasababishwa na uwazi uliobaki
baada kitu fulani kupotea toka kwa mtu ambacho alikuwa anakimiliki.
Mtu baada ya kuasi na kuupoteza utaratibu wa
ibada uliowekwa na Mungu pale Eden alianza kutafuta njia ya kuupata uwepo wa
Mungu.
Maana
mtu kwa jinsi alivyoumbwa hawezi kukaa nje ya uwepo wa Mungu, ni kama samaki
ukimtoa kwenye maji atakuwa na machaguo mawili kufa au kutafuta njia ya kurejea
kwenye maji ambayo ndo maisha yake (uzima wake) upo. Kwa hiyo na mtu kama
samaki ni lazima akae kwenye uwepo wa Mungu/Eden.
Sasa
basi huyu mtu akaanza kuitafuta Eden/uwepo wa Mungu, ndiyo tunaona dini
zinaanzishwa, dini zinagawanyika katika madhehebu n.k hii yote ni kuitafuta
Eden/uwepo wa Mungu.
Lakini
ukiangalia madhumuni ya dini zote yanafanana mfano wa mambo machache ni 1)dini
zote zinadai kwamba ni za kweli 2)zinadai zinamwamini Mungu 3) zinadai Mungu ni
mmoja 4) zinadai zina haki 5) zinadai zinaweza kutoa amani na utulivu 6)
zinadai zinaweza kutoa uwezo na nguvu 7) zinadai zenyewe ni bora kuliko
nyingine n.k.
Shida
ya dini zote badala ya kumuunganisha mwanadamu kwa nguvu na maarifa ya pamoja, dini
zimekuwa mgawanyaji mkuu wa wanadamu.
Dini
zote zinautaratibu wa kuendesha imani zao na zinatofautiana toka dini moja
kwenda dini nyingine kadhalika na madhehebu ya hizo dini. Na taratibu zote zina
lengo la kufikia kile kilichopotezwa kwenye bustani ya Eden.
Baadhi
ya taratibu ni vitu kama liturujia, madhabahu, mapokeo, jinsi ya kuwa mshirika
wa hizo dini mfano ubatizo, kusilimisha, kujaza fomu maalumu, kuunganishwa kwa
njia ya kutaja majina ya wanaukoo wote, viapo na nadhiri mbalimbali.
Lengo
la yote hayo ni kutafuta kilichopotea bustani ya Eden (uwepo wa Mungu) ili mtu
aweze kuishi.
DARAJA
KUELEKEA UFALME WA MUNGU/MBINGUNI ULIOREJESHWA NA YESU KUMREJESHA MTU KWA MUNGU
(WOKOVU)
Tukibaki
kwenye dini ni lazima mabishano, majigambo, kiburi, sifa, kujiona mwenye haki
zaidi ya dini nyingine kutatokea, lakini tukijadili kwa kufuata kusudi kuu la
Mungu mambo yatakwenda vizuri na hatimaye Mungu atatukuzwa.
Ukristo
(Christianity) kwa wanaofuata mpango wa Mungu wa Mwanzo 3:15 nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya
uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.
Ukristo sio DINI.UKRISTO ni uzima wa Mungu ndani ya Mtu, ni mfumo
kamili wa wa maisha yenye uzima wa Mungu ndani ya Mtu.
Kusudi kuu la Mungu linapatikana kwenye
Mwanzo 1:26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano
wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na
wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.
Kwa hiyo dhumuni/kusudi kuu
la Mungu kumuumba mtu ni ili KUTAWALA maana nyingine ni UFALME (sovereign rule).
Na hii ni kwa sababu Mungu alitaka kuongeza utawala wake usioonekana uje kwa
jinsi ya kuonekana kwa njia ya mwanadamu, kwa hiyo Mungu anataka kushirikiana
na sisi katika kutawala.
Tunachotakiwa kufanya ni kuifanya hii
dunia kuwa koloni la Mbinguni, mbinguni hakuna ujima, ukabaila, ubepari,
ubeberu, ujamaa, demokrasia. Mbinguni lugha ya utawala inayoeleweka ni Mfalme
na Ufalme na Wafalme. Wafalme wanatajwa hapa ni wote walioukubali huu mpango wa
Mungu kwenye Mwanzo 3:15.
Kwenye Mwanzo 3 kuna habari ya anguko la
mwanadamu hapo ndiyo mwanzo wa kuchanganyikiwa kwa wanaadamu katika mahusiano
yao na Mungu. Lakini pia tunaona Mungu akitangaza mpango wa kurejesha
alichokipoteza Adam, Mwanzo 3:15 nami nitaweka uadui
kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda
kichwa, na wewe utamponda kisigino.
UFALME WA MUNGU/MBINGUNI
ULIOREJESHWA NA YESU KUMREJESHA MTU KWA MUNGU (WOKOVU)
Ufalme
wa Mungu/mbinguni ni: Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki
na amani na furaha katika Roho Mtakatifu Rum 14:17
Pale
bustani ya Eden mtu alipoteza UFALME hakupoteza DINI, hili ni jambo la msingi
sana la kukumbukwa na kuelewa. Isaya 9:6 Inasema: Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa,
Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye
ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme
wa amani.
Unaona
huo unabii Isaya anautoa katika wakati uliotimilika, kimsingi Isaya alikuwa
anathibitisha kile Mungu alichokisema pale bustani ya Eden, Mwanzo 3:15 nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya
uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.
Tunaelewa kwamba Yesu Kristo ni kichwa
cha Kanisa, kwa maana hiyo sisi ni mwili ambao una mabega, kwa hiyo kwa lugha
rahisi uweza wa KIFALME tunaoambiwa na Isaya umerejeshwa kwetu. Atukuzwe Mungu
maana ahadi zake siku zote ni za kweli na neno lake, litokalo katika kinywa
mwake; halitamrudia bure, bali litatimiza mapenzi yake, nalo litafanikiwa
katika mambo yale aliyolituma Isaya 55:11.
Angalia Yohana anavyoanza mahubiri yake
Matayo 3:1-2 Siku zile aliondokea Yohana Mbatizaji
akihubiri katika nyika ya Uyahudi, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa
mbinguni umekaribia.
Kwa
sababu neno la Mungu halipingani, linatakiwa kuthibitishwa na mashahidi
wasiopungua wawili Yesu naye anaanza kazi yake kwa kukubaliana na Yohana
Mbatizaji, Mathayo 4:17 Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema,
Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
Kipaumbele
kikubwa cha Yesu ni kurejesha UFALME wa Mungu/Mbinguni kwa wanadamu, hebu
tuangalie mistari mbalimbali toka Injili kama ilivyoandikwa na Matayo, injili
nyingine Luka na Marko zimezungumzia pia ufalme wa mbinguni kwa uchache na
Matayo pia ametumia Ufalme wa Mungu kwa uchache lakini mimi nimependa kumtumia
Matayo.
Mathayo
3:2 Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
Mathayo 4:17 Tokea wakati huo Yesu
alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
Mathayo 5:3 Heri walio maskini wa roho;
Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Mathayo 5:10 Heri wenye kuudhiwa kwa
ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Mathayo 5:19 Basi mtu ye yote
atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo,
ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na
kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.
Mathayo 5:20 Maana nawaambia ya kwamba,
Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe
katika ufalme wa mbinguni.
Mathayo 6:9 Basi ninyi salini hivi; Baba
yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje,
Mathayo 7:21 Si kila mtu aniambiaye,
Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye
mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
Mathayo 8:11 Nami nawaambieni, ya kwamba
wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu,
na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;
Mathayo 10:7 Na katika kuenenda kwenu,
hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.
Mathayo 11:11 Amin, nawaambieni,
Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji;
walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye.
Mathayo 11:12 Tangu siku za Yohana
Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu
wauteka.
Mathayo 13:11 Akajibu, akawaambia, Ninyi
mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa.
Mathayo 13:24 Akawatolea mfano mwingine,
akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika
konde lake;
Mathayo 13:31 Akawatolea mfano mwingine,
akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu
akaipanda katika shamba lake;
Mathayo 13:33 Akawaambia mfano mwingine;
Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya
pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.
Mathayo 13:44 Tena ufalme wa mbinguni
umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona,
aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua
shamba lile.
Mathayo 13:45 Tena ufalme wa mbinguni
umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;
Mathayo 13:47 Tena ufalme wa mbinguni
umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna;
Mathayo 13:52 Akawaambia, Kwa sababu
hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye
nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.
Mathayo 16:19 Nami nitakupa wewe funguo
za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa
mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.
Mathayo 18:2 Ni nani basi aliye mkuu
katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao,
Mathayo 18:3 akasema, Amin, nawaambia,
Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Mathayo 18:4 Basi, ye yote
ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme
wa mbinguni.
Mathayo 18:23 Kwa sababu hii ufalme wa
mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.
Mathayo 19:12 Maana wako matowashi
waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi
waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa
matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na
alipokee.
Mathayo 19:14 Lakini Yesu akasema,
Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa
hao, ufalme wa mbinguni ni wao.
Mathayo 19:23 Yesu akawaambia wanafunzi
wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme
wa mbinguni.
Mathayo 20:1 Kwa maana ufalme wa
mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri
wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu.
Mathayo 22:2 Ufalme wa mbinguni
umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi.
Mathayo 23:13 Ole wenu waandishi na
Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi
wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie.
Mathayo
25:1 Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa
zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi.
Yesu
Kristo alisisitiza sana habari ya UFALME kwa sababu ndicho ambacho mwanadamu
alikuwa amepoteza na mwanadamu alikuwa katika harakati mbalimbali za kurejesha
kilichopotea tunaona kulikuwa na madhehebu mbalimbali kama vile Masadukayo,
Mafarisayo n.k, na wote hawa walikuwa wanatofautiana katika kurejesha kile kile
walichopoteza na walipingana kweli kweli na pia walimpinga na kumpa Yesu
changamoto mbalimbali ili kuonyesha wao ni bora zaidi.
Haya
madhehebu hayakuweza kushibisha kiu ya mwanadamu ya kurejesha kilichopotea, kwa
hiyo Mungu akakirejesha kwa kupitia mwanae mpendwa.
No comments:
Post a Comment
Barikiwa kwa ujumbe wako.