Thursday, July 2

SHERIA YA MUNGU INA MAAJABU

Zaburi 119:18 Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako.

Sheria ya Mungu ni mfumo wa kanuni, ambazo zimetolewa na Mungu mwenyewe ili kuratibu mahusiano baina yake na mwanadamu. Pia ni mkataba ambao Mungu ameundaa ili kumwongoza mwanadamu kupata ufalme wa mbinguni.
Katika sheria ya Mungu mwanadamu hajashiriki katika kuitunga hii sheria, anachotakiwa mwanadamu ni kuifuata kama ilivyo, maana Mungu ni upendo kwa hiyo sheria yake ni ya upendo.
Kwenye ufalme hamna demokrasia, ujamaa, ubepari, ujima, ukabaila wala mfumo wowote wa utawala unaoujua zaidi ya sheria ya KIFALME. Neno la Mfalme ni sheria ndiyo kusema neno la Mungu ni sheria na kitu cha ajabu kabisa Mungu mwenyewe hawezi kuwa juu ya neno lake. Hujanielewa nasema Mungu mwenyewe yupo chini ya Neno lake, Zaburi 89: 34 Mimi sitalihalifu agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu. Maana yake kama hawezi kuliahalifu wala kulibadili neno linalotoka kinywani mwake kwa hiyo yupo chini ya neno lake.
Ukiangalia sheria za kidemokrasia zinaanza kwa kusema ‘Sisi tumeamua hivi’ lakini sheria ya Mungu inasema ‘Mungu akasema’ ‘Mimi ni’ ‘Nime’. Kwa hiyo hapa hamna demokrasia ni sheria tu. Lakini ni sheria ambazo tukizifuata zinatuwezesha kula mema ya nchi na hatimaye uzima wa milele. Mungu pia ametushauri tuchague uzima, katika Kumbukumbu la Torati 30:19 Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako;
Msatari wetu wa ufunguzi una ombi kwa Mungu kwamba atufumbue macho yetu tuyaone maajabu yatokayo katika sheria yake.
Kumbe sheria ya Mungu ina maajabu, kwa hiyo tunatakiwa kumwomba Mungu atufumbue macho yetu tuyaone hayo maajabu. Yeremia 33:3 inasema: Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua. Bila kumwita/kumwomba Mungu hatuwezi kuona maajabu ya sheria yake.
Macho yetu yanahitaji kufumbuliwa ili kuweza kuona, mfano usipojua jinsi ya kumtii Mungu hutaweza kumpinga shetani, kwa hiyo inabidi kufumbuliwa macho ili uweze kujua jinsi ya kumtii Mungu ili uweze kumpinga shetani.
© Frank R.M Makundi

No comments:

Post a Comment

Barikiwa kwa ujumbe wako.